MILANGO ya neema imefunguka kwa wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Kila mfanyakazi ataweza kukopa kati ya Sh 100milioni na Sh 30milioni kulingana na wadhifa wake kwa ajili ya ujenzi wa nyumba. Habari ambazo Mwananchi imezipata zinasema kwamba mikopo hiyo itatolewa katika madaraja manane. Viwango hivyo vya mikopo ni vipya ambavyo vimetokana na maombi ya wafanyakazi hao ya kuongezewa kiasi cha mikopo hiyo kutoka katika kiwango cha awali walichokuwa wakipewa. Wafanyakazi wa daraja la chini kabisa, watakuwa wanakopeshwa Sh30milioni, wakati wafanyakazi wa ngazi ya juu kabisa watapata mkopo wa Sh100milioni. Wafanyakazi wa daraja la kwanza ambalo ni la juu kabisa na ambao watakuwa wanapata mkopo huo wa Sh100milioni ni pamoja na wakurugenzi, wakurugenzi washiriki na wataalamu washauri waandamizi. Daraja la pili ni la wafanyakazi wenye vyeo vya mameneja na wataalamu washauri ambao watapata mkopo wa Sh90milioni, wakati daraja la tatu linawahusisha mameneja wasaidizi na maafisa wakuu waandamizi (professional I) ambao wao watapata mkopo wa Sh70milioni. Daraja la nne linawahusisha wafanyakazi wenye vyeo vya maafisa wakuu (professional I) na maafisa wakuu waandamizi (professional II), ambao wao watajipatia mkopo wa Sh 60milioni, huku wafanyakazi katika daraja la tano ni wale wenye vyeo vya maafisa waandamizi (professional I) na maafisa wakuu (professional II) ambao watajipatia mkopo wa Sh 55milioni. Katika daraja la sita kuna wafanyakazi wenye vyeo vya maafisa ngazi ya III-I (professional I), maafisa waandamizi (professinal II) na maafisa- makarani wakuu (cleric officers) ambao watajipatia mkopo wa Sh45milioni. Daraja la saba ni la wafanyakazi wenye vyeo vya maafisa-makarani kuanzia ngazi ya III hadi ngazi ya maafisa-makarani waandamizi (cleric officers), makarani waandamizi na makarani wakuu (clerks) ambao wao watajipatia mkopo wa Sh40milioni. Daraja la nane ambalo ni la chini kabisa linawahusisha wafanyakazi wa taasisi hiyo ambao ni walinzi, wapishi, madereva, wahudumu wa ofisi na wa zahanati na makarani ngazi ya daraja la III-I ambao watapata mkopo wa Sh30milioni. Habari hizo zinasema kwamba viwango vya awali kwa wafanyakazi wa daraja la kwanza na la pili kama ilivyoainishwa hapo juu vilikuwa ni Sh50milioni, daraja la tatu vilikuwa Sh35milioni, daraja la nne na la tano Sh30milioni. Katika daraja la sita viwango vya awali vilikuwa ni Sh25milioni, daraja la saba walikuwa wakipata mkopo wa Sh20milioni wakati daraja la nane ambalo ni la chini walikuwa wakipata mkopo wa Sh15milioni. Kwa mujibu wa waraka uliosainiwa na Naibu Mwenyekiti wa Mfuko wa Mikopo ya Nyumba, Len Kisarika kwenda kwa wafanyakazi wote wa makao makuu na katika matawi ya Mwanza, Arusha, Mbeya, Zanzibar na Chuo cha Benki Mwanza kuwafahamisha kuridhia nyongeza hiyo, menejimenti hiyo imeridhia nyongeza hiyo ya mikopo ili kukidhi ongezeko la gharama za ujenzi. Katika waraka huo wa Desemba 2, mwaka huu ambao nakala yake imepelekwa kwa Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndullu na kwa Manaibu Gavana, menejimenti hiyo pia imeidhinisha ongezeko la kiwango cha mkopo kwa ajili ya matengenezo ya nyumba kutoka asilimia 15 hadi 20 ya mkopo uliotolewa. Waraka huo pia unabainisha kuwa kufuatana na hali ya Mfuko wa Mikopo ya Nyumba na ili kuhakikisha kuwa mikopo inayotolewa inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, utoaji wake umefanyiwa marekebisho kutegemea vipaumbele na masharti mbalimbali. Kwa mujibu wa waraka huo, kipaumbele cha kwanza ni kwa waombaji wapya, cha pili ni maombi ya nyongeza ya mikopo kwa ajili ya nyumba ambazo bado hazijakamilika na kipaumbele cha tatu ni maombi ya nyongeza ya mikopo kwa ajili ya uboreshaji wa nyumba. Masharti yaliyotajwa katika waraka huo kwa kipaumbele cha kwanza ni pamoja na salio la theluthi moja ya mshahara wa mwombaji baada ya makato, kama ilivyoainishwa kwenye Sheria ndogo za utumishi za (BoT Staff By Laws, 2008), uwezo wa mkopaji kurejesha mkopo na kuwasilisha hati ya kiwanja ambayo haijatolewa kama dhamana na isiyo na kikwazo chochote. Katika kipaumbele cha pili na cha tatu, mbali na masharti yanayotajwa katika waraka huo pamoja na masharti ya kwenye kipaumbele cha kwanza, kuna nyongeza ambayo ni pamoja na ukaguzi wa nyumba husika itakayofanyiwa uboreshaji kwa kipaumbele cha tatu. Masharti mengine ya kipaumbele cha pili ni ukaguzi wa nyumba husika ili kuthibitisha hatua iliyofikia katika ujenzi, tathmini ya thamani ya nyumba husika kutoka kwa mthamini wa majengo aliyesajiliwa, tathmini ya kamati ya kuthibitisha kama kiasi cha mkopo kinachoombwa kama kinatosheleza kukamilisha ujenzi wa nyumba husika.