Uwepo wa Site hii Unategemea sana Ushirikiano wangu na wako, na ni njia mojawapo ya kuonyesha mshikamano na Jamii inayotuzunguka , PLS Usisite kunitumia Habari au kitu chochote chenye Uhakika ambacho hisia zako zitakupeleka kuwa kitaleta Mabadiliko na mafunzo katika jamii, Kumbuka kuwa msaada si Fedha wala Lulu bali chochote kinachoweza kuleta mabadiliko katika Maisha ya mtu mwingine. Kwa lolote usisite kuwasiliana nami kupitia chingasite@gmail.com au tumainijhn@yahoo.co.uk au simu No. 0712221744 na 0787221744. Karibuni Wote
Powered By Blogger

Tuesday, May 25, 2010

Hukumu ya Liyumba ni kama Mazingaombwe!

MAHAKIMU kuwa katika jopo hakumaanishi kuwa katika kufikia uamuzi watafanana katika fikra, welewa na mtazamo na hilo limedhihirika katika hukumu dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba. Jopo hilo jana lilitofautiana na kuweka rekodi ambayo itakuwa ya mfano hata kwa wasomi wa sheria, baada ya Hakimu Edson Mkasimongwa kutofautiana na mahakimu wenzake Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa. Wote walikuwa wameunda jopo la kusikiliza kesi ya matumizi mabaya ya madaraka dhidi ya Liyumba, ambaye mahakimu Mlacha na Mwingwa walimwona ana hatia na hivyo kumhukumu kifungo cha miaka miwili jela. Lakini kwa upande wa Mkasimongwa, alimwona Liyumba kuwa hana hatia kwa kuwa mahakama ilishindwa kuthibitishiwa kama kweli alitumia madaraka yake vibaya katika ujenzi wa jengo pacha la BoT. Hata hivyo Mkasimongwa alisema kwa kuwa wengi wape, hukumu ambayo itahesabika kuwa ndio uamuzi wa mahakama itaanza kusomwa na kufuatia yake ambayo itabakia kuwa kumbukumbu ya mahakama na kuhifadhiwa katika jalada la kesi hiyo. Mkasimongwa katika uamuzi wake alisema mshitakiwa hana kesi ya kujibu kwa sababu mashitaka dhidi yake hayakuthibitishwa bila kuacha shaka yoyote kama sheria inavyotaka kwa kuwa kuna maswali mengi yalikosa majibu. Akisoma hukumu yake ambayo aliiita mbadala, alisema katika barua zilizoletwa mahakamani na upande wa mashitaka kama vielelezo zikidaiwa kusainiwa na mshitakiwa, hazina majibu kwamba ni kweli alifanya mabadiliko hayo na kama alikuwa na mamlaka hayo, vile vile haikuelezwa na upande wa mashitaka kuwa menejimenti nayo ilikuwa ikijibu nini. “Kuna uwezekano mabadiliko yale yaliridhiwa na Gavana na menejimenti yote, isingeleta swali kama kungekuwa na majibu au maelekezo tofauti,” alisema Mkasimongwa akiongeza kuwa ilitakiwa barua zilizokuwa zikimjibu mshitakiwa ziletwe, ili kujua na Utawala na Gavana walikuwa na uamuzi gani. Hivyo aliridhika kusema hakuna matumizi mabaya ya ofisi aliyotenda mshitakiwa. Hakimu Mlacha ambaye alisoma hukumu halisi alianza kwa kumkumbusha mshitakiwa mashitaka aliyofikishwa nayo mahakamani hapo ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 221. Hata hivyo mashitaka hayo yalifutwa na mahakama baada ya kukosa hatia wakati upande wa mashitaka ulipofunga ushahidi wake, pamoja na ya matumizi mabaya ya ofisi aliyokuwa amebaki nayo. Mlacha alisema katika hukumu hiyo aliyoanza kuisoma saa 3.50 hadi saa 7.20 mchana, kwamba bila shaka ushahidi ulionesha mshitakiwa alikuwa mtumishi wa umma katika kipindi chote cha mwaka 2001 hadi mwaka juzi kwenye Mradi wa 10 Mirambo (majengo pacha) anaodaiwa kubadili sura yake wakati ukitekelezwa, kwa mujibu wa mashahidi wanane walioletwa na upande wa mashitaka na wawili wa utetezi. Aidha alisema, mahakama inapingana na ushahidi uliotolewa na upande wa utetezi ambao ulitolewa na mshitakiwa na Bosco Kimela ambaye alikuwa Katibu wa Bodi ya BoT ambao walidai kuwa Liyumba hakuhusika na mabadiliko ya sura ya mradi na badala yake kuutupa mpira kwa Gavana wa wakati huo Daudi Ballali na Meneja wa Mradi, Deogratius Kweka. Katika ushahidi wao, walidai kuwa ingawa mradi ulikuwa chini ya kurugenzi yake, lakini mshitakiwa hakuhusika kutoa uamuzi. Vile vile mahakama haikubaliani na ushahidi wao kuwa Gavana alimteua mshitakiwa kwa mdomo, kusaini barua kwa niaba ya BoT, kwa kile walichodai kuwa Kweka hakuwa mwajiriwa wa kudumu wa benki hiyo. Hata hivyo, katika uamuzi wa mahakimu hao walikubaliana na ushahidi wa upande wa Serikali kwamba mawasiliano yoyote ya ndani ya ofisi za BoT yalifanyika kwa njia ya maandishi na si kwa mdomo kama Liyumba alivyodai kupewa jukumu la kusaini barua kwa mdomo huku kukiwa na ushahidi mwingine kwamba Gavana naye hakuwa na uamuzi wa mwisho bali Bodi ya Wakurugenzi. “Katika mradi huo uliolengwa kutekelezeka kwa mujibu wa mkataba, inakubalika kuwa haukutekelezeka kama ilivyotakiwa, yalikuwapo mabadiliko makubwa, ushahidi ulionesha kwamba katika matumizi yote ya maendeleo Bodi ndiyo ilikuwa na mamlaka ya mwisho, lakini katika mradi huu, kanuni hiyo haikufuatwa, fedha zililipwa bila utaratibu,” alisema Mlacha. “Mahakama inasema mshitakiwa alisaini barua zote zilizokuwa zikitoa maelekezo ya kubadili mradi na alifanya hivyo bila mamlaka kinyume cha sheria matumizi yaliyoongezeka na kuathiri BoT na bila shaka Taifa kwa jumla,” aliongeza. Baada ya mshitakiwa kuondolewa mahakamani, ndugu zake walilia huku wakidai kutoridhishwa na uamuzi huo. Hata hivyo wakili Majura Magafu anayemtetea Liyumba, alisema jana wangewasilisha notisi Mahakama ya Rufaa ili kuonesha nia yao ya kukata rufaa kwani ni imani yao kuwa ushahidi katika kesi hiyo haukuchambuliwa ipasavyo. Mtuhumiwa huyo alikaa rumande kwa zaidi ya mwaka mmoja na miezi mitatu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kutoa Sh bilioni 110. Akiwa katika basi linalobeba washitakiwa lenya namba STK 4373, saa 7.41 mchana Liyumba alianza safari yake akitokea Kisutu kuelekea makazi yake mapya ambako atatumikia kifungo hicho cha miaka miwili jela.
Chanzo:Habari leo

No comments:

VJN Super Motors

Wauzaji Mahiri wa Spare za Pikipiki na Magari yote toka Europe na Japan, Tupo Mtaa wa Msikitini Musoma Mjini, Pia tunaweza kutoa hudumu kwa watu wa Dar es salaam, Wasiliana nasi kwa Sanduku la Barua 557 Musoma, Simu No. 0282620610 , Barua pepe : vincent_nye@yahoo.co.uk. Karibuni wote