Uwepo wa Site hii Unategemea sana Ushirikiano wangu na wako, na ni njia mojawapo ya kuonyesha mshikamano na Jamii inayotuzunguka , PLS Usisite kunitumia Habari au kitu chochote chenye Uhakika ambacho hisia zako zitakupeleka kuwa kitaleta Mabadiliko na mafunzo katika jamii, Kumbuka kuwa msaada si Fedha wala Lulu bali chochote kinachoweza kuleta mabadiliko katika Maisha ya mtu mwingine. Kwa lolote usisite kuwasiliana nami kupitia chingasite@gmail.com au tumainijhn@yahoo.co.uk au simu No. 0712221744 na 0787221744. Karibuni Wote
Powered By Blogger

Monday, March 8, 2010

Makahaba zaidi ya 40,000 wajiandaa kuingia South Afrika kipindi cha Kombe la Dunia

Wanawake wapatao 40,000 wanatarajiwa kuingia nchini Afrika Kusini kufanya kazi ya ukahaba wakati wa mwezi mmoja wa kombe la dunia ambalo litafanyika baadae mwaka huu nchini humo.Afrika Kusini inaongeza ulinzi kwenye mipaka yake ili kuzuia wimbi hilo la makahaba ambao wengi wao wanatarajiwa kutoka nchi za ulaya mashariki.Zaidi ya watu 450,000 toka nchi mbali mbali duniani wanatarajiwa kuingia nchini Afrika Kusini kwaajili ya kombe la dunia.Akiongea katika kikao na umoja wa mataifa kuhusiana na vita dhidi ya madawa ya kulevya na uhalifu nchini humo, David Bayever, ambaye ni makamu mwenyekiti wa mamlaka ya kupambana na madawa ya kulevya nchini Afrika Kusini alisema kuwa maafisa wa Afrika Kusini wanahofia wimbi kubwa la wanawake wanaotarajiwa kuingia nchini humo kwa ajili ya biashara ya ukahaba."Tumepewa taarifa na waandaaji wa kombe la dunia kuwa wamepata taarifa kuwa wanawake 40,000 wameajiriwa kuja kufanya ukahaba wakati wa kombe la dunia", alisema."Hali inatisha sana kutokana na kwamba asilimia 16 ya idadi ya watu wana maambukizi ya virusi vya ukimwi", alisema.Bayever alisema kuwa wamehakikishiwa na idara ya uhamiaji kuwa ulinzi utaongezwa kwenye mipaka na ukaguzi wa pasport utaimarishwa.

Maalim Seif augua ghafla na kulazwa akisubiri ndege kwenda Oman

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad (pichani), ameugua ghafla wakati akijiandaa kupanda ndege kwenda Muscat, Oman. Baada ya kukatisha safari hiyo, Maalim Seif alipelekwa na kulazwa katika Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akiendelea kupata matibabu hadi jana jioni. Afya ya Maalim Seif ilianza kuzorota ghafla muda mfupi baada ya kuwasili katika uwanja wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere akitokea Zanzibar Ijumaa kwa ajili ya kupanda ndege. Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chama hicho, Ismail Jussa Ladhu, alithibitisha kuugua kwa kiongozi huyo. Ladhu ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa na mshauri wa Maalim Seif wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alisema kuwa kiongozi huyo alilazimika kupelekwa katika Hospitali ya Hindu Mandal baada ya kupata matatizo ya shinikizo la damu. “Ni kweli amesitisha safari baada ya kuugua ghafla akiwa katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere, isipokuwa anaendelea vizuri na matatibabu,” alisema Jussa jana alipozungumza na vyombo vya habari kuthibitisha taarifa za Maalim Seif kuugua ghafla juzi. Jussa alisema baada ya mwanasiasa huyo maarufu visiwani kufikishwa katika hospitali hiyo madaktari bingwa walichukua vipimo muhimu kabla ya kuamuliwa kumlaza. “Tayari madaktari wameshachukua vipimo muhimu ingawa tatizo linalo msumbua ni presha, lakini anaendelea vizuri na matibabu,” alisema Mkurugenzi huyo. Hata hivyo, Daktari anayemtibu kiongozi huyo, Dk. Ramaiya Kaosheki, alipotakiwa kueleza maendeleo ya mgonjwa wake, alisema hawezi kuzungumzia ugonjwa unaomsumbua Maalim Seif. “Bado amelazwa na anaendelea kupata matibabu ingawa siwezi kusema anasumbuliwa na maradhi gani ningependa hilo umuulize msaidizi wake,” alisema Dk. Kaosheki . Taarifa kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere zimeeleza kuwa Maalim Seif alilazimika kukimbizwa hospitali baada ya afya yake kubadilika ghafla na mwili kuanza kupoteza nguvu wakati akisubiri kuanza safari yake ya Oman. “Naweza kusema hali yake haikuwa ya kawaida kabla ya kuanza kupatiwa matibabu na baadaye madaktari kuamua alazwe ili apate matibabu zaidi,” kilieleza chanzo kimoja cha habari.

Michael Owen Kukaa nje msimu mzima!

Mshambulizi wa klabu ya soka ya Manchester United ya Uingereza, Michael Owen, akiwa na matatizo ya misuli ya paja, tangu mechi ya ushindi wa magoli 2-1 ya Kombe la Carling dhidi ya Aston Villa, hataweza kucheza tena msimu huu. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30, alifunga bao la kusawazisha katika mechi hiyo ya Wembley, lakini alipatwa na matatizo ya misuli alipokuwa akiukimbilia mpira katika kipindi cha kwanza. Kujeruhiwa kwa Owen kumempotezea matumaini yote ya kushirikishwa katika timu ya England. Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson, amesema kwamba kinyume na walivyofikiria hapo awali, hali ya Owen ni mbaya zaidi, na kwa kiasi fulani, alisema huenda hayo yalitokana na uwanja wa Wembley. Owen, ambaye ana mwaka mmoja uliosalia katika mkataba wake wa miaka miwili na Man U, awali alitazamiwa kupumzika kwa wiki chache tu. Atafanyiwa upasuaji Jumatatu.

Wanafunzi wawili wafa maji wakiogelea

WANAFUNZI wawili wa Shule ya Msingi Makabe, Livingston Richard (10)na mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Abdala (11), wamefariki dunia baada ya kuzidiwa na maji wakati wakiogelea. Watoto hao ambao walikuwa wakiongelea na wenzao katika Bwawa la Asili la linalojulikana kwa jina Rwegasira lilipo Mbezi Makabe jijini Dar es Salaam walifariki dunia baada ya kuzidiwa na maji. Kamanda wa polisi Mkoa wa Kinondoni, Elias Kalinga alisema tukio hilo, lilitokea juzi saa 11:30 jioni Makabe kwenye Bwawa la Asili linalojulikana kwa jina la Rwegasila. Kalinga alisema miili ya watoto hao, iliopolewa na wananchi wa eneo hilo, na maiti za watoto hao, zimehifadhiwa katika hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha na upelelezi wa dhidi ya vifo hivyo unaendelea. Katika tukio lingine, Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Ari iliyopo Tabata, Abdallah Miti (18), amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma za wizi wa Sh 5 milioni mali ya Anselem Sigela.

Wivu ni Kidonda Ukishiriki utakonda!

Mwanaume mwenye wivu aliyekuwa akiishi nchini Trinidad na Tobago Paul Bristol, 25 fundi wa vifaa vya umeme(pichani), alisafiri toka Trinidad and Tobago hadi Uingereza kumfuata mpenzi wake ambaye alipata mpenzi mwingine baada ya kufika Uingereza.Paul alifanya safari hiyo kutokana na wivu aliokuwa nao baada ya kuona picha ya mpenzi wake huyo kwenye mtandao wa Facebook akiwa na mwanaume mwingine aliyemtambulisha kama mpenzi wake. Paul alimuua kwa kumchoma choma na kisu Camille Mathurasingh, 27, ndani ya nyumba aliyokuwa akikaa mashariki mwa jiji la London. Paul amepandishwa kizimbani nchini Uingereza na alikanusha mashtaka ya mauaji aliyofunguliwa.Mahakama iliambiwa kuwa Paul na Camille walikuwa wapenzi kwa miaka mitatu nchini Tobago lakini Camille alivyofika Uingereza alipata mpenzi mwingine na kuamua kuuvunja uhusiano wake na Paul kimya kimya."Inavyoonekana mpenzi wake alitaka kuuvunja uhusiano wao kimyakimya bila ya kumwambia kuwa amepata mpenzi mwingine", alisema mwendesha mashtaka wa kesi hiyo."Aligundua uhusiano wao baada ya kuziona picha zao kwenye Facebook".Paul alikamatwa na polisi wakati alipokuwa akikimbia baada ya kufanya mauaji huku akiwa na damu usoni na kwenye nguo zake.

Wednesday, March 3, 2010

Msiba mkubwa Tabora

IDADI ya watu waliokufa kwenye ajali ya basi la AM Coach iliyotokea jumapili wilayani Nzega, imefikia 26, baada ya wengine wawili kufariki dunia juzi, huku maiti 18 wakitambuliwa na ndugu zao. Kutokana na kutambuliwa kwa miili hiyo, hadi kufikia juzi mchana, maiti wanane walikuwa hawajatambuliwa na wanaendelea kuhifadhiwa katika hospitali ya wilaya ya Nzega, kutokana na marehemu hao kutokuwa na vitambulisho vyovyote. Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Liberatus Barlow, maiti hao 18 walitambuliwa kwa vitambulisho vya kazi, vya kura na kadi za benki. Kamanda Barlow aliwataja waliotambuliwa hadi juzi kuwa ni Faustine Simon wa Katesh, Manyara; Pastory Kaiza; Epelanya Mleke; Gerald Nyitwe ambaye ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Kikosi cha 39 Arusha; Julieth Rupia wa Mwanza na Stephen Malolo wa Shinyanga. Wengine ni Noel Munisi; Paul Boniface wote wa Manyara; Ritha Thomas wa Moshi; Magreth Asenga (Moshi); Elizabeth Uriki ambaye ni Mtawa wa Kanisa Katoliki (Mwanza); Salome Richard (Babati); Doria Agai (Mwanza); Joachim Paul (Nzega); James Agai (Mwanza); Abeid Ngayanimo (Nzega), Milambo Benjamin (Nzega) na Benson Ochieng. Aidha, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Nzega, Dk. John Mombeki, alisema majeruhi wanne waliovunjika miguu na mikono walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza kwa tiba zaidi baada ya madaktari wa hospitali hiyo kukosa uwezo wa kutoa matibabu zaidi kwa majeruhi hao. Aliwataja majeruhi waliokimbizwa Bugando kuwa ni Nakijiwa Ibinga wa Same Kilimanjaro; Prosper Magacha (Hanang); Joyce Nyanda (Nyakato - Mwanza) na Chega Msila (Mwanza). Dk Mombeki alisema majeruhi wengine wawili waliokuwa wakikimbizwa pamoja nao kwenda Bugando, walifariki dunia njiani, hivyo kufanya idadi yao kuwa 26 baada ya juzi watu 24 kufa papo hapo katika ajali hiyo iliyotokea kati ya Kitangiri na Migua kiasi cha kilometa 12 kutoka Nzega mjini. Alisema kulingana na taarifa za kitabibu, majeruhi wengine sita wanatarajiwa kusafirishwa kwenda Bugando kwa matibabu zaidi. Akizungumzia majeruhi waliobaki hospitalini hapo, Mganga Mkuu wa Wilaya alisema wanaendelea vizuri na wamekuwa wakipata tiba kama inavyotakiwa na wakiendelea hivyo, wataruhusiwa kutoka siku chache zijazo. Katika hatua nyingine, imebainika kuwa mtoto ambaye hajatambuliwa jina, ni miongoni mwa majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo kupatiwa matibabu. Dk Mombeki alisema mtoto huyo amepewa uangalizi maalumu kutokana na umri wake kuwa mdogo kuliko wote walionusurika katika ajali hiyo na afya yake inaendelea vizuri. Inahisiwa kuwa mzazi au mlezi wake aliyekuwa akisafiri naye kwenye basi hilo alipoteza maisha. Alisema pamoja na mtoto huyo, pia watoto wengine mapacha wenye umri wa mwaka mmoja wamenusurika na wamelazwa hospitalini hapo. Mganga Mkuu aliwataja watoto hao kuwa ni Brighton na Brightness Juma ambao wanaishi na wazazi wao Mwanza ambapo pia mtoto mwenye umri wa miaka miwili, Mary Ochieng alinusurika. Hii ni ajali ya kwanza kutokea Tabora mwaka huu na kuua idadi kubwa ya watu aidha, ni ajali ya pili kubwa mwaka huu baada ya mabasi ya Chatco na Mzuri Trans kugongana uso kwa uso katika kijiji cha Kwangahu Handeni, Tanga na kuua watu 26.

Mazishi ya Kifahari yafanyika Dar

Mmoja wa wanzilishi wa shirika la kikristo la Salvation Army hapa nchini Major Nasson Kititu mwenye umri wa miaka 83 alizaliwa mwaka 1926 june 6 na amefariki dunia tarehe 26 februari katika hospitali ya Mikocheni, na kuzikwa katika shamba lake lililopo Kongowe Dar es Salaam,Alipata Kujiunga na Jeshi la wokovu mwaka1948 akiwa chunya alifunga ndoa na mke wake 'Maria Kititu' mwaka 1950 katika wilaya ya chunya mkoani mbeya,mwaka wa 1951 aliitikia wito wa kumtumiki mungu kama mchungaji akamua kwenda katika chuo cha uchungaji cha jeshi la wokovu Nairobi.Baada yakumaliza mafunzo ya uchungaji alianza kazi kama Luteni wa Jeshi la wokovu kanisa la Igunga 1952 hadi 1955Katika mazishi yake kulikuwa na mvua nyingi ilinyesha kuashiria kuwa alikuwa mtumishi wa mungu mamia ya waumini wakiwemo majirani ndugu jamaa walihudhulia katika mazishi ambayo hakika yalikuwa kama ya mtu mmoja wa kifahari kabisa na yenye heshima kuu kama mtumishi wa mungu yakiwa yameongozwa na COLONEL HEZEKIEL MAVUNDLA ambaye ni kiongozi wa Mkuu wa makanisa ya Salvation Army Tanzania.

Mvua ya siku mbili Dar yasababisha haya

Mamlaka yachunguza ajali ya ndege

MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imetuma timu ya wataalamu jijini Mwanza kuchunguza chanzo halisi cha ajali ya ndege aina ya Boeing 737 -200 namba BH-MVZ ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL). Aidha, Mamlaka hiyo imetangaza kuufunga uwanja wa ndege wa Mwanza kwa muda kwa ndege zote kubwa, hadi ndege hiyo itakapoondolewa eneo la tukio. Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Anga wa Mamlaka hiyo, John Njau, alisema jana Dar es Salaam kuwa mpaka sasa haijafahamika chanzo hasa cha ajali hiyo, ambayo ilisababisha ndege hiyo kuharibika hasa kwenye mguu wake wa kushoto. “TCAA tumetuma wataalamu wetu kuchunguza chanzo cha ajali, na watachokifanya ni uchunguzi wa awali kwa kuhoji marubani, abiria na mashuhuda, uchunguzi huo utatuwezesha kuiondoa ndege hiyo eneo la tukio na hivyo kufungua uwanja,” alisema Njau. Alisema wataalamu wawili ndio waliokwenda kuchunguza tukio hilo ambao ni rubani mkaguzi na mhandisi mkaguzi, ambao wataungana na timu ya wataalamu wengine wakaguzi kutoka idara za usafiri wa anga kuchunguza tukio hilo. Alisema mamlaka hiyo ina taarifa kuwa ndege hiyo ilipatwa na tukio la hatari juzi asubuhi wakati ikiwa katika mkimbio wa kusimama na kutokana na mvua ilitoka kwenye njia na kuingia kwenye ardhi tifutifu na wakati ikiendelea na mwendo huo, tairi lilirudi ndani na pua ya ndege kugusa chini. Alisema watu wote 46 wakiwamo wafanyakazi saba wa ndege hiyo walitoka salama. “Napenda kusisitiza kuwa ndege hii haikuanguka bali ilipatwa na tukio la hatari tu na mguu wake mmoja umeharibika vibaya, tunataka kujua sababu halisi.” Alisema TCAA imelazimika kufunga uwanja huo kwa ndege kubwa hasa zinazoweza kutumia umbali wa meta 2,000 hata kusimama kutokana na ndege hiyo ya ATCL bawa lake kuwa katikati ya njia ya ndege na hivyo kuruhusu ndege zinazotumia umbali wa meta 1,800 tu kusimama. Hata hivyo, hakusema uchunguzi huo utachukua muda gani ili kuwezesha uwanja huo kufunguliwa. “Siwezi kusema ni lini tutamaliza kuchunguza na kuiondoa ndege hii, siwezi kusema leo, kesho au keshokutwa.” Naye Meneja Masoko wa ATCL, Musyangi Kajeri, alisema kampuni hiyo pia imetuma wataalamu wake kuchunguza tukio hilo na kuangalia uwezekano wa kuendelea na huduma zake kama kawaida. Ndege hiyo ilipatwa na mkasa huo juzi asubuhi ikitoka Dar es Salaam kwenda Mwanza na wakati wa kutua ilivamia maji yaliyotokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha Mwanza ambayo kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa ATCL, William Haji, yaliingia kwenye injini moja na ilizima ghafla na kusababisha mtafaruku huo. ( Chanzo cha habari - Habari Leo)

Maisha bora kwa kila Mtanzania!

Hii ndio Hali halisi ndani ya ukuta wa majengo ya kituo cha Polisi cha Msimbazi kariakoo jijini Dar es salaam(Picha na Robert Okanda)

VJN Super Motors

Wauzaji Mahiri wa Spare za Pikipiki na Magari yote toka Europe na Japan, Tupo Mtaa wa Msikitini Musoma Mjini, Pia tunaweza kutoa hudumu kwa watu wa Dar es salaam, Wasiliana nasi kwa Sanduku la Barua 557 Musoma, Simu No. 0282620610 , Barua pepe : vincent_nye@yahoo.co.uk. Karibuni wote