Uwepo wa Site hii Unategemea sana Ushirikiano wangu na wako, na ni njia mojawapo ya kuonyesha mshikamano na Jamii inayotuzunguka , PLS Usisite kunitumia Habari au kitu chochote chenye Uhakika ambacho hisia zako zitakupeleka kuwa kitaleta Mabadiliko na mafunzo katika jamii, Kumbuka kuwa msaada si Fedha wala Lulu bali chochote kinachoweza kuleta mabadiliko katika Maisha ya mtu mwingine. Kwa lolote usisite kuwasiliana nami kupitia chingasite@gmail.com au tumainijhn@yahoo.co.uk au simu No. 0712221744 na 0787221744. Karibuni Wote
Powered By Blogger

Tuesday, October 27, 2009

Mshtakiwa wa Kesi ya EPA hoi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jana ilishindwa kusikiliza kesi ya wizi wa Sh 3.8 bilioni inayomkabili Farijala Hussein na wenzake baada ya mshtakiwa huyo kushindwa kusimama kizimbani kutokana na kusumbuliwa na tatizo la figo. Kesi hiyo ilipangwa kuendelea kusikilizwa mfululizo jana kwa mashahidi wa upande wa mashtaka, lakini Farijala ambaye alikuwepo mahakamani hapo alionekana amevimba uso na tumbo na hivyo kushindwa kusimama kizimbani. Wakili anayemtetea mshtakiwa huyo, Majura Magafu aliomba mahakama iahirishe kesi hiyo baada ya kudai kuwa mteja wake hataweza kukaa kizimbani kusikiliza kesi kutokana na kuumwa. Hata hivyo, wakili wa serikali, Frederick Manyanda alipinga hoja hizo na kudai kuwa si za msingi kwani upande wa utetezi ulipaswa kuithibitishia mahakama kwa kuonyesha vyeti.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, kiongozi wa jopo la mahakimu wanaosikiliza kesi hiyo, Samuel Karua aliahirisha kesi hiyo hadi leo ili kuangalia hali ya mshtakiwa huyo. Katika hatua nyingine, mshtakiwa wa pili, Rajabu Maranda jana aliwasilisha ombi mahakamani hapo la kutaka aruhusiwe kusafiri nje ya Dar es Salaam ili aende kwenye shughuli za kisiasa. Washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Ajay Somani, Imani Mwakosya, Esther Komu na Sophia Kalika. Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa waliiba zaidi ya Sh3 bilioni kutoka kwenye Akaunti ya malipo ya Madeni ya Nje (EPA) iliyokuwa Benki Kuu (BoT) baada ya kudanganya kuwa kampuni ya Mibare Farm imepewa deni na kampuni ya Textile Mills Ltd ya nchini India. Wakati huohuo, mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jana iliridhia maombi ya mfanyabiashara Jayant Kumar, maarufu kama Jeetu Patel, anayekabiliwa na kesi ya wizi wa Sh3.3 bilioni ya kutaka kesi hiyo isitishwe mahakamani hapo ili jalada liende Mahakama Kuu kwenye kesi aliyoifungua ya kikatiba. Akitoa uamuzi huo huku akinukuu kesi mbalimbali na vifungu vingine vya sheria, Hakimu Mkuu Mkazi Richard Kabate alisema upande wa mashtaka umeshindwa kutoa tafsiri sahihi kuhusu mwenendo wa kesi. Awali upande wa mashtaka ulipinga jalada hilo kupelekwa Mahakama Kuu baada ya kudai kwamba hoja za upande wa utetezi hazina msingi wowote kwani maneno yanayolalamikiwa ni ya mitaani na wala hayajaathiri mwenendo wa kesi hiyo.
Hakimu Kabate alisema kwa mujibu wa sheria Mahakama ya Kisutu haina uwezo wa kuyatolea maamuzi malalamiko yaliyotolewa na Jeetu. Katika malalamiko yake Jeetu anadai kuwa mwenendo wa kesi yao umeingiliwa kutokana na matamshi aliyoyatoa mwenyekiti mtendaji wa IPP, Reginald Mengi kwamba wao ni mafisadi papa. Alidai kuwa katika matamshi hayo ambayo yalitolewa kupitia kipindi maalumu kilichorushwa na kituo cha televisheni cha ITV, Mengi aliingilia uhuru wa mahakama kwa kuwahukumu wakati kesi yao bado inaendelea mahakamani.
Alidai kuwa kutokana na matamshi hayo jamii iliwaona wao wana hatia dhidi ya tuhuma zinazowakabili. Tayari mahakama ya Kisutu imeridhia kusitishwa kwa kesi nyingine mbili zinazomkabili Jeetu na wenzake ili majalada ya kesi hizo yapelekwe Mahakama Kuu kwenye kesi ya kikatiba aliyoifungua. Kesi hiyo itatajwa Novemba 6 mwaka huu. Jeetu, Devendra Patel na Amit Nandy wanadaiwa kuiibia BoT Sh 3.3 bilioni baada ya kudanganya kuwa kampuni yao ya Navy Cut Tobacco (T) Ltd imepewa deni hilo na kampuni ya Matsishuta ya nchini Japan.

No comments:

VJN Super Motors

Wauzaji Mahiri wa Spare za Pikipiki na Magari yote toka Europe na Japan, Tupo Mtaa wa Msikitini Musoma Mjini, Pia tunaweza kutoa hudumu kwa watu wa Dar es salaam, Wasiliana nasi kwa Sanduku la Barua 557 Musoma, Simu No. 0282620610 , Barua pepe : vincent_nye@yahoo.co.uk. Karibuni wote