
“Bunge linapokuwa kwenye mchakato wa kutaka Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru achukuliwe hatua, kisha taasisi hiyo ikaanza kuwahoji wabunge wanaosubiri utekelezaji wa maagizo waliyoyatoa, ni kinyume cha utawala wa sheria,” alisema. Kwa mujibu wa Mwakyembe, watendaji wa Takukuru walianza kuwahoji wabunge mbalimbali katika kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja, wakitaka taarifa kuhusu madai ya wabunge kupewa posho wanapotembelea taasisi za umma, licha ya kulipwa stahiki zao na ofisi ya Bunge. Dk. Mwakyembe alisema hatua iliyochukuliwa na Takukuru kuwahoji wabunge, inatia mashaka hasa kwa vile taasisi hiyo imewahi kuwalipa posho wabunge mara kadhaa. Kwa upande mwingine, Dk. Mwakyembe alisema watuhumiwa wa ufisadi wanatumia baadhi ya vyombo vya habari (akivitaja jina) kuwachafulia majina wananchi wanaotetea maslahi mapana ya umma. “Si jambo la ajabu nilivyoandikwa na gazeti la (analitaja jina), hili linamilikiwa na mafisadi, linatetea maslahi ya mafisadi kiasi cha kupoteza mvuto wake kwa wasomaji,” alisema mbunge huyo machachari.
Suala la kuhojiwa kwa wabunge kuhusiana na posho wanazodaiwa kuchua mara mbili, kwenye Bunge na kwa taasisi wanakofanya kazi, linaelezwa kuwa ni juhudi za kutaka kupunguza makali ya wabunge. Jana baadhi ya wabunge waliozungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao, walisema wanaona mbinu hizi kama mapambano ya kitaasisi. Takukuru mwishoni mwa wiki walitoa taarifa kwa vyombo vya habari wakisema wabunge kama walivyo wananchi wengine wanawajibika kuitikia mwito wao wa kuhojiwa katika masuala mbalimbali yanaohusiana na rushwa.
No comments:
Post a Comment