Uwepo wa Site hii Unategemea sana Ushirikiano wangu na wako, na ni njia mojawapo ya kuonyesha mshikamano na Jamii inayotuzunguka , PLS Usisite kunitumia Habari au kitu chochote chenye Uhakika ambacho hisia zako zitakupeleka kuwa kitaleta Mabadiliko na mafunzo katika jamii, Kumbuka kuwa msaada si Fedha wala Lulu bali chochote kinachoweza kuleta mabadiliko katika Maisha ya mtu mwingine. Kwa lolote usisite kuwasiliana nami kupitia chingasite@gmail.com au tumainijhn@yahoo.co.uk au simu No. 0712221744 na 0787221744. Karibuni Wote
Powered By Blogger

Monday, October 19, 2009

Vita Ya Ufisadi yageuka Shubiri

VITA ya ufisadi iliyotangazwa na baadhi ya wabunge waliojipambanua kuwa ni wapambanaji wa ufisadi na kuungwa mkono na baadhi ya watu hivi sasa inaonekana kuwa shubiri kutokana na baadhi ya maamuzi yaliyofanywa kwa hofu ya ufisadi kuonekana kuigharimu nchi kiasi cha kuhatarisha ustawi wa kiuchumi na kijaami.
Uhasama baina ya wabunge na mawaziri wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ulioonekana katika Bunge lililopita kiasi cha kuilazimisha Halmashauri Kuu ya chama hicho kuunda kamati maalum ya kutafuta suluhu ni miongoni mwa mambo yaliyochangiwa kwa kiasi kikubwa na vita hiyo ambayo hivi sasa imeacha majeraha makubwa nchini.
Uchunguzi wa Tanzania Daima Jumapili pamoja na mahojiano iliyofanya na baadhi ya viongozi mbalimbali imeonyesha baadhi ya maamuzi nyeti yanashindwa kupata baraka za viongozi wa kisiasa ambao hivi sasa wamekuwa wakitaka kushindana na kukomoa pasi na kuangalia athari za maamuzi yao.
Kukomoa huko ndiko kunakomtikisa Rais Jakaya Kikwete pamoja na kamati aliyoiunda chini ya Rais mstaafu, Alli Hassan Mwinyi, ambayo imeshaanza kuonyesha kutokuwa na uwezo uliotarajiwa kutatua suala hilo linaloonekana kuizidi kimo CCM.
Chuki miongoni mwa wabunge na mawaziri wa CCM sasa imeonekana si kukitafuna chama bali hata mgawo wa umeme uliopo ambao baadhi ya watendaji shirika la ugavi wa umeme nchini (TANESCO) walishatoa mapendekezo kadhaa serikalini ili kuinusuru nchi kuingia katika janga hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Dk. Idris Rashid, ni mmoja wa watendaji waliosimama kidete kuelezea mipango yao ya kuboresha uzalishaji wa umeme ikiwemo kununua mitambo mipya, kununua ya Dowans na mingine ambayo ilikumbana na vikwazo vikali.
Baada ya Dk. Idris kupata upinzani huo alitangaza kuwa TANESCO imejitoa kununua mitambo ya Dowans huku akionya kuwa shirika hilo lisije likalaumiwa kwa mgawo ambao ungejitokeza Oktoba na Novemba mwaka huu.
Onyo hilo la Dk. Idris lipokewa kwa shutuma nzito na baadhi ya wanasiasa wakiongozwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo ilidai bora nchi iingie gizani kuliko kununua mitambo hiyo.
Mgawo wa umeme ulioanza wiki iliyopita wa saa 14 kwa siku ndiyo umewafanya baadhi ya wananchi, wanasiasa, wafanyabiashara kukumbuka onyo la Dk. Idris na kuwalaumu viongozi walioshiriki kwa namna moja au nyingine kukwamisha mipango ya TANESCO.
Wakati mgawo wa umeme ukionekana kushika kasi Kamati ya Nishati na Madini, chini ya Mbunge wa Bumbuli, William Shelukindo (CCM), itangaza kufanya uchunguzi ili kuona kama mgawo huo umesababishwa na watendaji wa TANESCO ili kutimiza mipango yao hasa ya kununua mitambo ya Dowans.
Kamati hiyo ilizungumza na watendaji wa TANESCO na baadaye ilisalimu amri kuwa mgawo huo ulitokana na kuharibika kwa mashine kadhaa pamoja na upungufu wa maji kama ambavyo shirika hilo lilivyotangaza.
Baadhi ya wafanyabiashara wenye viwanda wameingiwa na hofu ya kuendelea kufanyabiashara hasa kutokana na mgawo huo ambao umeathiri kwa kiwango kikubwa uzalishaji.
Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI) ni miongoni mwa wadau waliojitokeza kutaka nchi isiendelee kuwa gizani kwa kuendekeza maamuzi yenye athari ilhali kuna mitambo yenye uwezo wa kuzalisha umeme lakini inashindwa kutumika.
Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) ni miongoni mwa taasisi za serikali zinazoathirika na mgawo huo kwa kuwa imekuwa ikipoteza mapato mbalimbali iliyokuwa ikiyapata kutokana na uzalishaji mali.
Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wameweka bayana kuwa nchi ipo hatari kuporomoka zaidi kiuchumi kama serikali haitochukua hatua za haraka kutafuta vyanzo vya kudumu vya kuzalisha nishati ya umeme ambayo hutegemewa na viwanda mbalimbali.
Wakati wachambuzi hao wakitoa tahadhari hiyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, ambaye siku za nyuma alijitokeza hadharani kulitaka Bunge na serikali kufikiria upya juu ya mitambo ya Dowans na ikiwezekana wainunue ili nchi isiingie gizani ameibuka tena kuitaka serikali itaifishe mitambo hiyo.
Zitto alisema uamuzi wa kuitaifisha mitambo hiyo ni mgumu lakini kwa hali ilivyo hivi sasa ni lazima viongozi wakubali kufanya umuzi huo hata kama watasakamwa na wahisani kwa kukiuka sheria.
Hoja hiyo ya Zitto kwa kiasi kikubwa imeonekana kuungwa mkono na kada mbalimbali za wananchi huku serikali kupitia kwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, akikataa kufanya hivyo kwa madai ni kukiuka sheria za nchi.
Kauli hiyo ya Ngeleja imeonekana kupingwa na baadhi ya watu wakiwemo wanasheria ambao wameweka bayana kuwa serikali imekuwa ikikiuka sheria mbalimbali ambapo wakati mwingine si kwa manufaa ya walio wengi hivyo ni vema kufikiria upya wazo la Zitto.
Tindu Lissu ni mmoja wa wanasheria aliyeweka wazi kuwa serikali haiwezi kuwa na kesi ya kujibu kama ikifikia hatua hiyo kwa kuwa sheria ya kimataifa ya uwekezaji pamoja na namna mitambo hiyo ilivyoingia hapa nchi imegubikwa na mizengwe.
Mwanasheria ameweka bayana kuwa hofu hiyo ya serikali haipaswi kupewa nafasi katika kipindi hiki ambacho nchi ipo hatarini kuporomoka kiuchumi kutokana na kushuka kwa uzalishaji viwandani.
Mgawo wa umeme umeonekana kuibua upya sakata la vita ya ufisadi ambalo lilishika kasi baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa kutokana na kuhusishwa katika kashfa ya kuipa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharula kampuni ya Richmond ambayo ilibainika kutokuwa na uwezo.
Sakata la Richmond ndilo kwa kiasi kikubwa lililozaa ufa na makundi yenye kuhasimiana vikali ndani na nje ya Bunge kiasi cha kuhatarisha mustakabali wa CCM ambao katika siku za hivi karibuni umekumbwa na kashfa mbalimbali.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaona serikali itakuwa na wakati mgumu wa kuamua kipi cha kufanya kumaliza tatizo la mgawo wa umeme ambalo kwa namna moja au nyingine lilisababishwa na utendaji usio makini pamoja na tamaa za watu waliopewa jukumu la kuongoza nchi.
Moja kati ya sababu inayowafanya wachambuzi hao kuiona serikali kuwa iko njia ni ukweli kuwa wabunge walio katika mstari wa mbele kupinga baadhi ya mambo ni kutoka CCM ambacho ndicho chama kilichoshikilia dola.
Wachambuzi hao pia hawakusita kueleza wakati mgumu itakaokumbana nao Kamati ya Mzee Mwinyi iliyopewa jukumu la kutatua uhusiano mbovu baina ya wabunge na mawaziri ulioshamiri hivi sasa.
Ugumu wa Kamati ya Mzee Mwinyi unadaiwa utachagizwa zaidi na joto la uchaguzi mkuu ambapo kila mbunge anataka kuonekana anawajibika kwa wananchi wake hivyo kuwawia vigumu viongozi wa serikali. (Habari toka Mtanzania Daima)

No comments:

VJN Super Motors

Wauzaji Mahiri wa Spare za Pikipiki na Magari yote toka Europe na Japan, Tupo Mtaa wa Msikitini Musoma Mjini, Pia tunaweza kutoa hudumu kwa watu wa Dar es salaam, Wasiliana nasi kwa Sanduku la Barua 557 Musoma, Simu No. 0282620610 , Barua pepe : vincent_nye@yahoo.co.uk. Karibuni wote