Uwepo wa Site hii Unategemea sana Ushirikiano wangu na wako, na ni njia mojawapo ya kuonyesha mshikamano na Jamii inayotuzunguka , PLS Usisite kunitumia Habari au kitu chochote chenye Uhakika ambacho hisia zako zitakupeleka kuwa kitaleta Mabadiliko na mafunzo katika jamii, Kumbuka kuwa msaada si Fedha wala Lulu bali chochote kinachoweza kuleta mabadiliko katika Maisha ya mtu mwingine. Kwa lolote usisite kuwasiliana nami kupitia chingasite@gmail.com au tumainijhn@yahoo.co.uk au simu No. 0712221744 na 0787221744. Karibuni Wote
Powered By Blogger

Tuesday, March 16, 2010

Hatima ya Liyumba kujulikana April 9

Upande wa mashtaka katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 221.1 za mradi wa majengo pacha ya Benki Kuu Tanzania (BoT), umefunga ushahidi wake dhidi ya kesi hiyo inayomkabili Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki hiyo, Amatus Liyumba, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam. Baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake Mahakama hiyo imesema, itatoa uamuzi kama Liyumba ana kesi ya kujibu au la Aprili 9, mwaka huu. Wakili wa Serikali Mwandamizi, Juma Ramadhani, alidai jana mbele ya jopo la mahakimu watatu wakiongozwa na Edson Mkasimongwa, Lameck Mlacha na Benedict Muingwe, wanaosikiliza kesi hiyo, kuwa baada ya upande wa Jamhuri kuita mashahidi wanane na kuwasilisha vielelezo 13 mahakamani hapo, umeamua kufunga ushahidi. Ramadhani alidai kuwa ili kesi iendelee kwa mujibu wa Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai, kifungu cha 131 cha sheria ya mwaka 2002, upande wa mashitaka umefunga ushahidi wao dhidi ya kesi hiyo. Hata hivyo, wakili wa utetezi, Majura Magafu, aliomba mahakama hiyo kusikiliza majumuisho ya mwenendo wa kesi kwa maneno ili iweze kuona kama mshitakiwa ana kesi ya kujibu au la. Kadhalika, upande wa Jamhuri ulitoa pingamizi la kufanya majumuisho hayo jana kwa maneno na uliomba mahakama hiyo kuruhusu hoja za majumuisho zitolewe kwa maandishi ili kusaidia mahakama kutoa uamuzi. “Kwa sababu kesi hii ni ya Jamhuri, tunaomba tupewe nafasi ya kutoa hoja zetu kwa maandishi ili tuweze kuishahiwishi mahakama kama mshtakiwa ana kesi ya kujibu dhidi ya tuhuma zinazomkabili,” alisema Ramadhani. Hata hivyo, baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, mahakama hiyo iliamuru ziwasilishwe kwa maandishi. Upande wa utetezi utawasilisha hoja zao Machi 22, mwaka huu na upande wa mashitaka utajibu Machi 29, mwaka huu. Hatima ya Liyumba kama ana kesi ya kujibu ama la itajulikana Aprili 9, mwaka huu baada ya mahakama kutoa uamuzi. Mapema Januari 10, mwaka jana, Liyumba na aliyekuwa Meneja Mradi huo, Deogratius Kweka, walipandishwa kizimbani katika mahakama hiyo wakikabiliwa na mashitaka ya kutumia madaraka vibaya na kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha. Hata hivyo, mahakama hiyo Aprili mwaka jana, iliwafutia mashtaka hayo, lakini Liyumba alifikishwa tena mahakamani akikabiliwa na tuhuma hizo. Awali, shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo, Mpelelezi Seif Mohamed (49), aliiambia mahakama kwamba Liyumba alikuwa akifanya mabadiliko ya kuongeza gharama za mradi na baadaye kuijulisha bodi ya BoT. Kadhalika, alidai kuwa Liyumba alifanya mabadiliko hayo baada ya kutoa maelekezo kwa njia ya barua kwa Mhandisi mshauri wa mradi huo. Shahidi wa pili, Meneja wa musuala ya bodi Yusto Tolola (45) kutoka BoT, alidai mahakamani kwamba bodi ilipokea maombi ya nyongeza ya mabadiliko ya fedha za mradi wakati tayari matumizi yameshafanyika. Pia, shahidi huyo alidai kuwa kurugenzi iliyokuwa ikiongozwa na Liyumba ilikuwa ikiomba kibali cha kufanya mabadiliko ya mradi wa ujenzi wakati tayari matumizi ya fedha yamekwisha kufanywa. Shahidi wa tatu, Julius Angelo (49) ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Fedha BoT, alimtetea Liyumba kwamba aliidhinisha malipo madogo ya nyongeza katika mradi wa ujenzi wa majengo pacha kulingana na cheo alichokuwa nacho. Aidha, Mkurugenzi huyo aliiambia mahakama kwamba malipo makubwa ya nyongeza ya mradi huo, yaliidhinishwa na aliyekuwa Gavana wa BoT, Daudi Balali. Shahidi wa nne, aliyekuwa Mkurugenzi wa bodi ya BoT, Michael Shirima (66), alidai kuwa alitaka kujiuzulu, baada ya kumjulisha aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati huo, Basil Mramba, kuhusu matumizi makubwa ya mradi wa majengo pacha, yaliyofanyika bila kibali cha bodi hiyo ambapo alijibiwa kwamba asingeweza kuingilia uamuzi wa Balali kwa kuwa anawajibika kwa Rais aliyemteua. Kadhalika, alidai kuwa alifikia maamuzi ya kujiuzulu baada ya kuona hakuna mchango anaoutoa kwa bodi hiyo ambayo ilipelekewa kuidhinisha mapendekezo ya matumizi ya fedha za mradi wakati tayari malipo yamefanyika bila mamlaka ya bodi hiyo. Katika kesi hiyo, Liyumba anadaiwa kuwa akiwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala, alipindisha mkataba wa BoT kuhusu mradi wa ujenzi wa maghorofa pacha na hivyo kuongeza kiasi cha fedha zilizokuwa zikihitajika katika ujenzi. Ilidaiwa kuwa kutokana na Liyumba kupindisha mkataba huo, aliisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 153,077,715.71 ambazo ni sawa na Sh. 221,197,299,200.96 kwa sasa.

No comments:

VJN Super Motors

Wauzaji Mahiri wa Spare za Pikipiki na Magari yote toka Europe na Japan, Tupo Mtaa wa Msikitini Musoma Mjini, Pia tunaweza kutoa hudumu kwa watu wa Dar es salaam, Wasiliana nasi kwa Sanduku la Barua 557 Musoma, Simu No. 0282620610 , Barua pepe : vincent_nye@yahoo.co.uk. Karibuni wote