Uwepo wa Site hii Unategemea sana Ushirikiano wangu na wako, na ni njia mojawapo ya kuonyesha mshikamano na Jamii inayotuzunguka , PLS Usisite kunitumia Habari au kitu chochote chenye Uhakika ambacho hisia zako zitakupeleka kuwa kitaleta Mabadiliko na mafunzo katika jamii, Kumbuka kuwa msaada si Fedha wala Lulu bali chochote kinachoweza kuleta mabadiliko katika Maisha ya mtu mwingine. Kwa lolote usisite kuwasiliana nami kupitia chingasite@gmail.com au tumainijhn@yahoo.co.uk au simu No. 0712221744 na 0787221744. Karibuni Wote
Powered By Blogger

Tuesday, March 9, 2010

Mke wa Balozi auwawa kinyama Dar

Mke wa Balozi mwandamizi mstaafu wa Tanzania nchini Marekani, Andrew Daraja, ameuawa kinyama kwa kuchomwa kisu cha kifuani sehemu ya titi la kushoto na polisi wanamtafuta mhudumu wa shamba, James Mabakuri (22), kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Elias Kalinga, alimtaja mke huyo wa balozi kuwa ni Anna Daraja, mkazi wa Kimara Temboni, jijini Dar es Salaam. Kamanda Kalinga aliyaaambia baadhi ya vyombo vya habari kuwa mauaji hayo yalitokea juzi nyumbani kwa Balozi Daraja Temboni, jijini Dar es Salaam wakati balozi akiwa safarini mkoani Tanga. Kamanda Kalinga alisema kuwa mtuhumiwa huyo ambaye wanaendelea kumtafuta, mara baada ya tukio hilo anadaiwa kuiba kiasi ya Sh. milioni 2 na kutoweka nazo bila kuchukua kitu kingine. Akisimulia zaidi tukio hilo, Kamanda Kalinga alisema Februari 14, mwaka huu Balozi Daraja alimuaga mke wake kuwa anasafiri kwenda Muheza, Tanga na kumuacha na mhudumu wa shamba ambaye alikuwa akiishi kwenye nyumba hiyo. Alisema wakati Balozi Daraja akiwa safarini, kijana huyo anadaiwa kuwa alimchoma Anna kisu kwenye titi la kushoto na kufa papo hapo. Alisema mtuhumiwa baada ya kuhakikisha mama huyo amekufa alianza kufanya upekuzi kwenye nyumba hiyo, ikiwemo chumbani kwa balozi. Alisema mtuhumiwa huyo mara baada ya kuzikuta fedha hizo sehemu zilipokuwa zimehifadhiwa, alitoweka eneo la tukio na kwenda kusikojulikana. “Nyumba hiyo ilikuwa na vitu vyenye thamani kubwa, lakini inaelekea mtuhumiwa hakuwa na nia navyo, alichukua fedha na kutokomea nazo,” alisema Kamanda Kalinga. Kamanda Kalinga alisema kuwa upekuzi uliofanywa kwenye chumba cha mtuhumiwa kilichopo nje ya nyumba kubwa ya balozi huyo kulikutwa nguo za aina mbalimbali pamoja na vitu vingine. Alisema nguo hizo ni mali ya mtuhumiwa. Alisema uchunguzi wa awali uliofanyika kwenye nyumba hiyo, umebaini kuwa mtuhumiwa huyo alifanya kitendo hicho cha kikatili usiku kutokana na mazingira waliyoyakuta.
“Tukio hili lingefanyika mchana huyu mama angepata msaada, lakini inaonyesha wazi kuwa mtuhumiwa alimvizia usiku ndipo akafanya mauaji hayo,” alisema Kamanda Kalinga. Alisema juhudi za kumsaka mtuhumiwa huyo katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam na nje ya mkoa zinaendelea. Kamanda Kalinga alisema mtuhumiwa huyo inadaiwa kuwa aliletwa na fundi ujenzi ambaye hajafahamika jina lake kwa ajili ya kazi alizokuwa akizifanya. Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa uchunguzi zaidi. Akizungumza kwa njia ya simu , Balozi Daraja alisema wakati wa tukio la kuuawa kwa mke wake alikuwa safarini mkoani Tanga. “Jana (juzi) niliporudi nyumbani kutokea Tanga nilipofika kwenye geiti la nyumba yangu, niligonga muda mrefu bila mafanikio,” alisema. Alisema mara baada ya kufanikiwa kuingia ndani (bila kuelezea aliingiaje), aliukuta mwili wa mke wake ukiwa umelala kwenye gereji huku kisu kikiwa kimechomwa kwenye titi. Alisema hadi sasa hafahamu mtu aliyefanya kitendo hicho na kwamba uchunguzi unaendelea.

No comments:

VJN Super Motors

Wauzaji Mahiri wa Spare za Pikipiki na Magari yote toka Europe na Japan, Tupo Mtaa wa Msikitini Musoma Mjini, Pia tunaweza kutoa hudumu kwa watu wa Dar es salaam, Wasiliana nasi kwa Sanduku la Barua 557 Musoma, Simu No. 0282620610 , Barua pepe : vincent_nye@yahoo.co.uk. Karibuni wote