Uwepo wa Site hii Unategemea sana Ushirikiano wangu na wako, na ni njia mojawapo ya kuonyesha mshikamano na Jamii inayotuzunguka , PLS Usisite kunitumia Habari au kitu chochote chenye Uhakika ambacho hisia zako zitakupeleka kuwa kitaleta Mabadiliko na mafunzo katika jamii, Kumbuka kuwa msaada si Fedha wala Lulu bali chochote kinachoweza kuleta mabadiliko katika Maisha ya mtu mwingine. Kwa lolote usisite kuwasiliana nami kupitia chingasite@gmail.com au tumainijhn@yahoo.co.uk au simu No. 0712221744 na 0787221744. Karibuni Wote
Powered By Blogger

Friday, March 26, 2010

Vilio, Simanzi vyatanda katika mji mdogo wa Kibamba Dar es salaam

Vilio, simanzi na majonzi, vilitawala jana katika eneo la Kibamba nje kidogo ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam, wakati miili ya abiria 11, ukiwamo wa mama mjamzito, ikinasuliwa kutoka kwenye vyuma vya daladala na lori la mafuta ya taa, baada ya magari hayo kugongana uso kwa uso na watu hao kufariki dunia papo hapo. Miili ya watu hao ilinasa katika vyuma hivyo baada ya lori hilo aina ya IVECO lenye namba za usajili T 189 ABP kuligonga daladala hilo aina ya Toyota Hiace lenye namba za usajili T 615 AJW na kisha kulisukuma kwenye mtaro na kulilalia hivyo kufanya kazi ya kuinasua miili hiyo kutoka kwenye vyuma vya magari hayo kuwa ngumu. Daladala hilo linalofanya safari kati ya Mlandizi na Ubungo, lilikuwa likitokea Kibamba wakati lori hilo linalomilikiwa na Mahmoud Mohamed lilikuwa likisafirisha lita 30,000 za mafuta ya taa kutoka Dar es Salaam kwenda Isaka, Shinyanga. Ajali hiyo inayotajwa kuwa moja ya ajali mbaya zilizowahi kutokea jijini Dar es Salaam katika siku za karibuni, ilitokea saa 10:30 alfajiri jana, baada ya lori hilo kutaka kulipita gari lililokuwa mbele yake na kwenda upande wa pili wa barabara ya Morogoro na kuligonga daladala hilo. Kutokana na ajali hiyo, daladala hilo liliharibika vibaya kiasi cha kukutofaa tena kwa matumizi na watu wote 11, wanaume wakiwa wanane na wanawake watatu waliokuwamo walifariki dunia papo hapo na miili yao iliharibika vibaya. Baadhi ya maiti zilishuhudiwa zikiwa zimepasuka vichwa na nyingine viungo vya miili vikiwa vimekatika vipande vipande. Miongoni mwa waliokuwamo kwenye daladala hilo, ni pamoja mama mjamzito, aliyefahamika kwa jina la Zainabu Ally, ambaye pembeni ya mwili wake kulikutwa mkoba uliokuwa na vifaa vinavyotumika wakati wa kujifungua. Haikufahamika mara moja iwapo mama huyo safari yake ya jana kabla ya kukumbwa na umauti, alikuwa akienda hospitali kujifungua au la. Maiti mwingine aliyetambuliwa ni dereva wa daladala hilo, Faraji Ismail Ngalamba, ambaye alikutwa akiwa amenasa kwenye vyuma vya lori hilo. Alinasuliwa baada ya askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji cha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na wafanyakazi wa Chama cha Msalaba Mwekundu pamoja na polisi kukata vyuma vya lori hilo. Mwingine, ni abiria Shukuru, ambaye alitambuliwa na baba yake mzazi, Hussein Saleh Mwagilo, mkazi wa Kibamba katika eneo la ajali na mwingine alitambuliwa kwa jina la Abutwalib Twaibu. Ajali hiyo ilivutia maelfu ya wakazi wa maeneo ya katikati na nje ya Jiji la Dar es Salaam, ambao walifurika katika eneo la ajali kushuhudia miili ya watu iliyonasa kwenye vyuma vya magari hayo kwa takriban saa 8; kuanzia saa 10:00 alfajiri hadi saa 6:10 mchana. Askari polisi wa kawaida na wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), usalama barabarani pamoja na askari kanzu wenye silaha za moto, wakiongozwa na Kamanda wa Kikosi cha Askari wa Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, walifika saa 1:00 asubuhi na kudhibiti eneo lote la ajali. Hatua hiyo ilichukuliwa na polisi, baada ya baadhi ya watu kuvamia eneo hilo muda mfupi baada ya ajali kutokea na kuanza kuiba mafuta kutoka kwenye tanki la lori hilo. Kazi ya kuinasua miili kutoka kwenye vyuma vya magari hayo, ilianza rasmi saa 4:30 asubuhi baada ya gari la kampuni ya Effco Crane la kunyanyua vitu vizito kufika eneo hilo. Kazi hiyo iliyochukua zaidi ya saa mbili; kuanzia saa 4:30 asubuhi hadi saa 6:10 mchana, ilisababisha barabara ya Morogoro kufungwa kwa muda huo. Hata hivyo, awali kazi hiyo ilichelewa kuanza baada ya askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji cha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kufika mapema, lakini wakashindwa kufanya lolote kutokana na kuwa na vifaa duni. Hali hiyo ilidhihirika pia, wakati kazi ya kunasua miili hiyo ikifanyika, kwani askari wa kikosi hicho walishuhudiwa wakibeba miili ya watu hao huku wakiwa wamevaa mifuko ya plastiki ya rangi nyeusi badala ya glovu. Maiti mbili; moja ya Shukuru Hussein, nyingine ya mwanamke, ambaye hajatambuliwa pamoja na mguu, baada ya kunasuliwa zilichukuliwa na Land Rover ya polisi na kupelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali Teule ya Tumbi, Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani. Maiti nyingine tisa, ambazo hadi tunakwenda mitamboni zilikuwa hazijatambuliwa, zilipelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam. Wakati kazi ya kuinasua miili hiyo ikiendelea, watu waliofika eneo la ajali, walianza kushangilia baada ya mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina la Fred Nicodemus, mkazi wa Kibamba, kuangua kilio ghafla katika eneo, ambako lori na daladala hilo zilikuwa zimeanguka. Fred aliangua kilio baada ya kuitambua maiti ya mama yake mzazi, Ester Christiano, aliyekuwa mfanyabiashara wa Kariakoo, jijini Dar es Salaam. Baada ya kusikia sauti ya Fred ikitoka katika eneo yalikokuwa magari hayo, umati wa watu hao walianza kushangilia wakidhani kijana huyo alikuwa miongoni mwa abiria aliyetolewa akiwa hai katika vyuma vya magari hayo baada ya kunusurika katika ajali hiyo. Awali, mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Rashid Mfaume, alisema daladala lililopata ajali, lilianza safari Kibaha na inakisiwa walikuwamo abiria kati ya saba hadi 10. Shuhuda mwingine, Frank Msemwa, ambaye ni dereva wa gari la wanafunzi, alisema aliona lori lililosababisha ajali likitaka kulipita gari lililokuwa mbele yake na baada ya dakika chache ikatokea ajali hiyo. Baba mzazi wa marehemu Shukuru, Hussein Saleh Mwagilo, alisema mwanaye mauti yamemfika alipokuwa njiani akienda kuchukua gari kwa tajiri yake kwa ajili ya kufanya kazi. Naye Sajenti Solomon Mwangamilo, ambaye anaishi karibu na eneo ilikotokea ajali hiyo, alisema akiwa nyumbani kwake saa 11:00 alafajiri, alisikia kishindo kikubwa. Alisema aliposikia hivyo, alijua pengine ni ajali ya kawaida, hata hivyo, hakupuuza, bali alivaa sare kisha akatoka na kwenda kwenye eneo la ajali na kuona watu wakiwa wamekandamizwa na magari hayo. Kamanda Mpinga akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la ajali, alisema walifanikiwa kudhibiti eneo la ajali baada ya baadhi ya watu kutaka kuiba mafuta kutoka kwenye tangi la lori lililopata ajali. Alisema lori hilo lilikuwa limebeba lita 30,000 za mafuta ya taa na kwamba kazi ya kunasua maiti za watu waliokufa ilichelewa kuanza kutokana na magari matatu ya kunyanyua vitu vizito yaliyofika mapema kushindwa kufanya kazi hiyo kutokana na kuwa na vifaa duni. “Hii ni changamoto kubwa inayoikabili serikali,” alisema Kamanda Mpinga, ambaye alisema taarifa za awali alizopata zilieleza kuwa waliokufa ni watu wanane.

No comments:

VJN Super Motors

Wauzaji Mahiri wa Spare za Pikipiki na Magari yote toka Europe na Japan, Tupo Mtaa wa Msikitini Musoma Mjini, Pia tunaweza kutoa hudumu kwa watu wa Dar es salaam, Wasiliana nasi kwa Sanduku la Barua 557 Musoma, Simu No. 0282620610 , Barua pepe : vincent_nye@yahoo.co.uk. Karibuni wote