
SERIKALI ya Namibia imemtunuku Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere nishani ya heshima. Nishani hiyo alikabidhiwa mkewe, Mama Maria ikiwa ni utambuzi na kuthamini nafasi yake katika harakati za kupigania uhuru wa Afrika ikiwemo nchi yao . Alikabidhiwa nishani hiyo juzi pamoja na watu wengine sita mashuhuri waliotoa mchango mkubwa kwa Namibia na kufanikisha ipate Uhuru Machi 21, 1990 kutoka kwa Afrika Kusini. Walipewa tuzo hizo wakati wa chakula cha usiku kilichoandaliwa na Rais Hifikepunye Pohamba kwa ajili ya marais wote na wageni wengine waalikwa waliofika nchini hapa, akiwemo Rais Jakaya Kikwete kushuhudia sherehe za miaka 20 ya Uhuru pamoja na kuapishwa kwa Rais na Waziri Mkuu nchini hapa. Akielezea umuhimu wa Namibia kumtunuku Mwalimu Nyerere, Msimamizi wa Itifaki katika hafla hiyo, Martin Anyamba alisema kuwa mamilioni ya Waafrika, jina la Nyerere litaendelea kuwa kwenye kumbukumbu zao na wataendelea kumheshimu. Alisema Nyerere alikuwa mwanafalsafa, kiongozi na kiunganishi cha watu na mtu mwenye busara aliyefanya kazi kubwa ya kufungua mipaka ya nchi yake kwa ajili ya kupigania uhuru wa nchi mbalimbali barani. Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Rais Jakaya Kikwete, ilielezwa kwamba ushirikiano na umoja wa Namibia uliowezesha kupata uhuru, ulitokana na mchango mkubwa wa Tanzania ambayo ilijitoa mhanga kwa ajili yao . “Wanachama wengi wa SWAPO walipata mafunzo huko Kongwa ( Dodoma )…Mwalimu Nyerere alikuwa muumini mzuri wa umoja,” alisema Anyamba kabla ya kumuita Mama Maria aliyekuwa wa kwanza kati ya watu saba kutunukiwa, kitendo kilichoshangiliwa kwa makofi na vigelegele na umati uliohudhuria. Wengine waliokabidhiwa nishani hizo kutokana na mchango wao katika uhuru wa Namibia ni Rais Mstaafu wa Zambia , Kenneth Kaunda aliyekwenda kuipokea kwa mbwembwe akitembea kwa mwendo wa haraka. Wakati huohuo Umoja wa Wanawake Watanzania waishio Namibia kupitia kwa Mwenyekiti wao, Chiku Mnubi, juzi walimpa Mama Nyerere zawadi ya ramani ya nchi hiyo ikiwa ni utambuzi wa mchango wake katika uhuru na pia kumshukuru kufika nchini humo kuhudhuria sherehe za Uhuru na kuapishwa kwa Rais Pohamba.
No comments:
Post a Comment