Uwepo wa Site hii Unategemea sana Ushirikiano wangu na wako, na ni njia mojawapo ya kuonyesha mshikamano na Jamii inayotuzunguka , PLS Usisite kunitumia Habari au kitu chochote chenye Uhakika ambacho hisia zako zitakupeleka kuwa kitaleta Mabadiliko na mafunzo katika jamii, Kumbuka kuwa msaada si Fedha wala Lulu bali chochote kinachoweza kuleta mabadiliko katika Maisha ya mtu mwingine. Kwa lolote usisite kuwasiliana nami kupitia chingasite@gmail.com au tumainijhn@yahoo.co.uk au simu No. 0712221744 na 0787221744. Karibuni Wote
Powered By Blogger

Monday, March 15, 2010

MAUAJI YA DEREVA TAKSI:Ndugu wakosa imani na Kamanda Kova

FAMILIA ya dereva wa taksi ambaye inadaiwa aliuawa kwa kipigo akiwa kituo cha polisi, imepinga taarifa ya kamanda wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Suleman Kova kuwa kijana huyo alifariki dunia wakati akipelekwa Hospitali ya Temeke. Tamko la familia hiyo linatokana na taarifa iliyotolewa na Kova kwa waandishi wa habari mwishoni mwa wiki kuwa dereva huyo, Mussa Juma, 27, aliwaambia polisi waliokuwa wakimuhoji Machi 10 kuwa anajisikia vibaya na ndipo walipoamua kumkimbizia kwenye hosptali hiyo, lakini akafariki dunia akiwa njiani. Kamanda Kova, hata hivyo, alisema taarifa sahihi za kifo chake zitatolewa baada ya daktari kuufanyia uchunguzi mwili wake. Lakini msemaji wa familia ya dereva huyo, Mwinjuma Mzee aliliambia gazeti hili jana kuwa kauli hiyo ya Kova inalenga kupotosha ukweli wa tukio hilo na pia kuishinikiza tume iliyoundwa na polisi mkoani Temeke kutoa majibu yasiyoweza kupingana na ya kiongozi wao wa kanda. Alisema wakati kiongozi mkubwa kama huyo anapozungumza maneno kama hayo, inatia shaka moja kwa moja kuwa hata tume aliyoiunda italazimika kutoa majibu yasiyopingana naye. Alisema ndugu wa marehemu pamoja na msimamzi wake aliyemwakilisha tajiri walishuhudia kijana huyo akihojiwa hadi majira ya saa 8:00 usiku wakati alipokuja kuchukuliwa na doria nyingine (Tembo 42) na kupelekwa kusikojulikana," alisema Mzee. Mzee alisema ushahidi mwingne unaoonyesha kuwa kijana wao alifariki Machi 8 mwaka huu, yaani siku aliyokamatwa, na si Machi 10 kama inavyoelezwa na Kamanda Kova, ni kurudi kwa askari kutoka kikosi hicho aliyemchukua kijana huyo na kutoa taarifa kwa mkubwa wake kuwa kazi imekwisha. "Ndugu walioshuhudia kisa hicho wanathibitisha kuwa askari aliyekuja kumchukua usiku wa saa 8:00 baada ya muda alirudi na kumweleza bosi wake akisema 'kazi imekwisha'. kauli hiyo inatosha kuwa ni uthibitisho wa kuwa kijana huyo alifariki usiku wa Machi 8 na si Machi 10 kama alivyosema Kamanda Kova," alisema. Kutokana na hofu kuwa polisi walitaka kuchukua vipimo kwenye mwili wa kwa kushtukiza siku ya Ijumaa, familia hiyo imehamisha maiti hiyo kutoka Hospitali ya Temeke na sasa uchunguzi utafanyika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Mzee alisema lengo la kuhamisha mwili huo ni ukweli kwamba madaktari bingwa wa taaluma ya upasuaji na wenye uzoefu wa uchunguzi wa kijinai wapo Muhimbili. Alisema sababu ya pili ni kutaka kukwepa njama zinazoweza kufanywa na polisi wa kituo cha Changaombe ambao wanatuhumiwa kuhusika kumpiga kijana huyo. Wakili wa familia hiyo, Ibrahim Bendera ambaye anafuatilia mambo yote yanayohusu mkasa huo, alimuandikia barua mganga mkuu wa Hosptali ya Temeke akimweleza nia ya kuhamisha mwili huo na kuupeleka Muhimbili. Katika hatua nyingine, baadhi ya polisi ambao inadaiwa walihusika kumshambulia kijana huyo, wanadaiwa kuanza kuwatafuta ndugu wa marehemu kwa lengo la kutaka kusuluhisha suala hilo nje ya msingi ya kisheria. Mzee alithibitisha kuwapo kwa taarufa hizo na kusema hata namba na majina ya askari hao wanayo. "Kumekuwa na usumbufu mkubwa kwa baadhi ya ndugu wa familia... baadhi ya polisi wamekuwa wakiwapiguia simu wanandugu kwa lengo la kuomba msamaha na kutaka suala hilo liishe nje ya msingi ya kisheria," alidai Mzee. Hadi sasa familia hiyo imeshindwa kuendelea na taratibu za mazishi ikisubiri matokeo ya uchunguzi wa maiti hiyo.
(Chanzo cha habari - Mwananchi)

No comments:

VJN Super Motors

Wauzaji Mahiri wa Spare za Pikipiki na Magari yote toka Europe na Japan, Tupo Mtaa wa Msikitini Musoma Mjini, Pia tunaweza kutoa hudumu kwa watu wa Dar es salaam, Wasiliana nasi kwa Sanduku la Barua 557 Musoma, Simu No. 0282620610 , Barua pepe : vincent_nye@yahoo.co.uk. Karibuni wote