Uwepo wa Site hii Unategemea sana Ushirikiano wangu na wako, na ni njia mojawapo ya kuonyesha mshikamano na Jamii inayotuzunguka , PLS Usisite kunitumia Habari au kitu chochote chenye Uhakika ambacho hisia zako zitakupeleka kuwa kitaleta Mabadiliko na mafunzo katika jamii, Kumbuka kuwa msaada si Fedha wala Lulu bali chochote kinachoweza kuleta mabadiliko katika Maisha ya mtu mwingine. Kwa lolote usisite kuwasiliana nami kupitia chingasite@gmail.com au tumainijhn@yahoo.co.uk au simu No. 0712221744 na 0787221744. Karibuni Wote
Powered By Blogger

Wednesday, February 17, 2010

Haya ni mauaji ya kinyama - Watu 17 wa Ukoo mmoja wauawa kwa Sime Musoma

WATU 17 wa familia tatu za ukoo mmoja, wamefariki dunia na wengine watano kunusurika baada ya kushambuliwa usiku wa manane na kundi la watu waliokuwa na silaha za jadi. Habari zilizolifikia jana zimeeleza kuwa tukio hilo lillitokea saa 6:00 usiku wa kuamkia jana katika kitongoji cha Mgarajabo Buhare Musoma mjini mkoani Mara. Kwa mujibu wa habari hizo zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Robert Boaz, mbali na mauaji hayo, wauaji hao pia waliua ng'ombe wa jamaa za marehemu hao. Kamanda Boaz alitaja moja ya familia zilizofikwa na mkasa huo kuwa ni ya Kawawa Nyarukende ambako watu wanane waliuawa ndani ya nyumba hiyo na yeye mwenyewe kujeruhiwa vibaya na amelazwa katika hospitali ya Mkoa wa Mara. Kwa mujibu wa kamanda huyo, familia nyingine iliyovamiwa ni ya Mgaya Nyarukende ambayo watu wawili waliuawa na yeye kujeruhiwa. Familia ya Morisi Mgaya ambako waliuawa watu saba. "Watu wote waliouawa ni wa ukoo mmoja na ndio maana unaona majina yanafanana," alisema Kamanda Boaz na kuongeza: "Ndani ya nyumba ya Morisi Mgaya waliuawa watu saba na yeye kujeruhiwa vibaya. Wauaji hao walikuwa wanatumia vitu vyenye bapa kali kama mapanga na sime". Kamanda Boaz aliwataja waliouawa kuwa ni Nyasinde Morisi, Mgaya Morisi, Mage Morisi, Maheri Morisi, Allice Morisi na Kado Morisi. Wengine ni Kawawa Kinguye, Angelina Kawawa, Kinguye Kawawa, Mengi Kawawa, Nyarukende Kawawa, Juliana Kawawa, Nyambona Kawawa, Nyanyama Kawawa, Dorika Mgaya, Umbera Mgaya na mwanafunzi wa sekondari ya Mkirara, Sospeter Sopereti ambaye alikuwa mgeni wa familia hiyo. "Nadhani walikuwa watu wengi maana nyumba zile zimetawanyika sana moja iko umbali wa kama mita 300, hivyo isingewezekana wamalize kufanya unyama hapa halafu waende kwingine,"alisema kamanda. Alisema uchunguzi wa awali umebaini kwamba, baada ya mauaji hayo hakukuwa na tukio lolote la wizi hali inayoonyesha kuwa huenda mauaji hayo yamefanyika ili kulipiza kisasi. Hata hivyo baadaye jana kamanda Boaz alilieleza kuwa polisi inawashikilia watu watano kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo huku wakiendelea na msako wa kuwatafuta wengine. Kamanda Boaz :"Hivi sasa ni mapema kuwataja watuhumiwa. Kwanza kazi bado inaendelea na kufanya hivyo itakuwa ni kuharibu upelelezi". Muuguzi Mkuu wa hospitali ya mkoa wa Mara, Benedictor Mwijarubi alikiri kupokea majeruhi wanne wa tukio hilo na kufahamisha kuwa majeruhi mmoja alikufa muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo. Alibainisha kuwa Dorika Siti (70) alifia hospitalini hapo kwa sababu ya kuvuja damu nyingi kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata sehemu mbalimbali mwilini. Muuguzi huyo aliwataja majeruhi waliofikishwa hospitalini hapo kuwa ni Morisi Mugaya (40) Maximilliani Roba (20) na Maria Kawawa (18), alisema hali za majeruhi hao sio nzuri na madaktari wanaendelea na jitihada kuokoa maisha yao. Akinukuu maelezo ya majeruhi hao, muuguzi huyo alisema tukio hilo lilitokea kwa wauaji hao kuvunja milango ya wenyeji wakiwa wamelala. Alisema watoto wawili wadogo walipona baada ya kulala katikati ya maiti na hivyo kudhaniwa kuwa wamekufa. Alisema majeruhi hao walipona baada ya kupiga kelele na watu kuanza kujitokeza kutoa msaada kulikowafanya wauaji kukimbia. Wakizungumza na gazeti hili kutoka eneo la tukio, baadhi ya mashuhuda walisema mauaji hayo yamefanyika kulipa kisasi kufuatia tukio linalodaiwa kutokea mwaka 2006 ambapo watu wawili wa kabila la Wazanaki waliuawa katika jaribio la wizi wa mifugo kwenye familia hizo. Kwa mujibu wa mashuhuda hao ambao hawakutaka kutajwa , ndugu wa marehemu hao walilaani mauaji hayo na kusema ndugu zao hawakuwa wezi wa mifugo bali wawindaji wa nungunungu na nguruwe pori. Inadaiwa kuwa katika tukio hilo la mwaka 2006, Kawawa ambaye jana alivamiwa nyumbani kwake, alikamatwa akihusishwa na tukio la mwaka huo , lakini baadaye aliachiwa huru. Kabla ya kuvamiwa jana, akiwa mahabusu kwa tuhuma za tukio la mwaka 2006, watu wasiojulikana walifika nyumbani kwake na kufanya mauaji ya watu wawili kisha wakaondoka. Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Enock Mfuru alisema limetokana na kulipizana visasi na akaliagiza jeshi la polisi kuhakikisha linawasaka na kuwatia mbaroni wahusika wote aliosema wameuchafua mji wa Musoma. Tukio hilo limeufanya mji mzima wa Musoma kuzizima kwa simanzi huku wengi wakidai kuwa wahusika watakuwa wanafahamika kwa kuwa tukio hilo ni mwendelezo wa matukio ya tangu mwaka 2005 walipouawa watuhumiwa wa wizi wa mifugo.

No comments:

VJN Super Motors

Wauzaji Mahiri wa Spare za Pikipiki na Magari yote toka Europe na Japan, Tupo Mtaa wa Msikitini Musoma Mjini, Pia tunaweza kutoa hudumu kwa watu wa Dar es salaam, Wasiliana nasi kwa Sanduku la Barua 557 Musoma, Simu No. 0282620610 , Barua pepe : vincent_nye@yahoo.co.uk. Karibuni wote