
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete, ametangaza juhudi zake za kulinda maslahi ya wasanii nchini kwa kuunda kikosi maalumu cha kulinda haki zao na pia amewafungulia studio ya kisasa kwaajili ya kazi zao. Rais Kikwete alitoa ahadi hizo juzi alipoungana na wasanii mbalimbali nchini katika tamasha la Zinduka, kwa ajili ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria nchini.Katika tamasha hilo ambalo lilifanyika katika viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam, majira ya jioni, liliweza kuteka umati wa mashabiki, kufuatia kuwa ni mara ya kwanza kufanyika nchini.Wasanii zaidi ya 20 kutoka Tanzania na nje ya Tanzania waliweza kukonga nyoyo mashabiki hao kwa jinsi walivyoliumudu jukwaa.Rais aliwatoa hofu wasanii na kuwapongeza kwa jinsi walivyoweza kujipanga na kufanya jambo la msingi la kuelimisha umma, “Ningependa mjue kuwa, mimi nyimbo na kazi zenu zote nazifuatilia, nyimbo za Bongo fleva mimi ni msikilizaji mzuri sana, Zamani mimi nilikuwa nacheza Sikinde, Soboso na Lumba, kwa nyimbo za Bongo fleva ya sasa mnanikosha sana nawapa hongera” alisema JK.Wakati akisoma hotuba ya uzinduzi huo, Kikwete aliwataka wasanii wote nchini kujithamini na kuthamini kazi zao ili ziweze kuwanufaisha. “Kilio chenu, nimekisikia siku nyingi juu ya kunyonywa kwa mapato ya kazi yenu, najua mnavuja jasho lakini hamfaidiki matunda yake naahidi kuendelea kulishughulikia” alisema Kikwete.Rais aliwataka wasanii kujipanga na kutimiza malengo waliyojipangia, huku akiwataka kuitumia mitambo mipya na ya kisasa ya studio ambayo aliwaahidi kipindi cha nyuma kuwaletea ambapo alitimiza ahadi hiyo.“Kilio chenu cha studio ya kisasa mlichokuwa mnalia muda mrefu nimewatimizieni, mshindwe wenyewe na kwa swala la kuibiwa kazi zenu na kuwafanya kukosa mapato naahidi kulitokomeza kabisa hilo kwa kuunda kikosi maalum cha kushugulikia kero zote” Aliendelea kusema kuwa, kwa wasanii wa filamu na muziki ndiyo wanoongaza kwa kudhulumiwa kazi zao, huku akiwataka kusubiri neema kwa uundwaji wa kikosi kazi ‘Task force’ maalum kitakachokuwa chini ya Wasanii wenyewe, COSOTA, TRA, BASATA, Jeshi la Polisi na wizara yenye dhamana kuhakikisha kero hizo zinapotea kabisa nchini.
No comments:
Post a Comment