Uwepo wa Site hii Unategemea sana Ushirikiano wangu na wako, na ni njia mojawapo ya kuonyesha mshikamano na Jamii inayotuzunguka , PLS Usisite kunitumia Habari au kitu chochote chenye Uhakika ambacho hisia zako zitakupeleka kuwa kitaleta Mabadiliko na mafunzo katika jamii, Kumbuka kuwa msaada si Fedha wala Lulu bali chochote kinachoweza kuleta mabadiliko katika Maisha ya mtu mwingine. Kwa lolote usisite kuwasiliana nami kupitia chingasite@gmail.com au tumainijhn@yahoo.co.uk au simu No. 0712221744 na 0787221744. Karibuni Wote
Powered By Blogger

Monday, February 22, 2010

Mganga 'feki' aliyeua wanne ahukumiwa kunyongwa

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa, mganga wa kienyeji 'feki' Mabala Masasi, mwenyeji wa Shinyanga, baada ya kupatikana na hatia ya makosa manne ya mauaji ya kukusudia. Masasi mwenye wake wanane na watoto 32, alipatikana na hatia ya kuwaua kwa makusudi Shija Mihayo na mkewe Fatuma Makunja, Mustafa Masanja na Mohamed Makwaya wote wakazi wa kijiji cha Chamakweza Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani kinyume cha kifungu cha 196 cha kanuni ya adhabu (Penal Code). Akisoma hukumu ya kesi hiyo ya jinai namba 75 ya mwaka 2006, Ijumaa iliyopita, Jaji Raziah Sheikh alisema baada ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka na ushahidi wa upande wa utetezi aliridhika kuwa upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa pasi na shaka yoyote. "Nimeridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha bila shaka na naunga mkono maoni ya wazee wawili wa baraza waliosema kuwa mshtakiwa ana hatia. Nimeridhika kuwa mshtakiwa wa kwanza (Masasi) pekee au na wenzake wasiokuwepo mahakamani waliwaua marehemu hao kama inavyodaiwa na upande wa mashtaka; Hivyo kwa maoni yangu mshtakiwa una hatia ya kuwaua marehemu (watu) wanne kinyume cha sheria kifungu cha 196 cha Kanuni za Adhabu," alisema Jaji Sheikh na kumpa nafasi wakili wa mshtakiwa Oscar Msechu kusema jambo lolote kabla ya kutamka adhabu. Wakili Msechu aliomba mahakama imuonee huruma na kumpunguzia adhabu mshtakiwa kwa madai kuwa ana wake wanane na watoto 32 ambao wote wanamtegemea na kwamba hilo ni kosa lake la kwanza na muda aliokaa rumande (miaka takribani 7) ni mingi, utetezi ambao hata hivyo Jaji Sheikh aliutupilia mbali. "Ninavyofahamu kisheria adhabu kwa kosa la kuua kwa makusudi ni moja tu nayo ni kunyongwa. Hivyo nami ninatoa adhabu ya kunyongwa hadi kufa. Mshtakiwa anayo haki ya kukata rufaa," alisema Jaji Sheikh na kunyanyuka kwenye kiti chake. Kabla ya hukumu hiyo ilidaiwa na upande wa mashtaka kuwa mshtakiwa aliwaua watu hao kwa nyakati tofauti tofauti, kati ya mwezi Februari na mwezi Mei, mwaka 2004, kwa lengo la kuchukua mali walizokuwa nazo. Ilidaiwa kuwa kabla ya kuwaua watu hao mshtakiwa aliwadanganya kuwa yeye ni mganga wa kienyeji mwenye uwezo wa kuwatibu magonjwa mbalimbali na pia kuwapa dawa ya kupata utajiri, lakini baada ya kuwanywesha dawa hizo waliishiwa nguvu na kudhoofika ndipo akawapiga hadi kuwaua kabla ya kuwafukia ardhini. Upande wa mashtaka ulidai kuwa mshtakiwa huyo ambaye alikuwa ni mgeni kijijini hapo alifikia nyumbani kwa marehemu Shija na kuwadanganya kuwa yeye ni mganga wa kienyeji ana tibu magonjwa mbalimbali kwa kutumia dawa za kienyeji na kwamba ana dawa za kuwafanya wawe matajiri. Ilidaiwa kuwa marehemu Shija na mkewe walimuamini akawanywesha dawa, lakini mara tu baada ya kunywa dawa hiyo waliishiwa nguvu na kulegea ndipo mshtakiwa alipowapiga kwa mchi wa kutwangia vichwani hadi wakafariki dunia. Baada ya kuwaua ilidaiwa kuwa mshtakiwa aliwazika kwenye kisima kilichokuwa kimekauka nyuma ya nyumba yao. Upande wa mashtka uliendelea kudai kuwa baadaye marehemu Masanja na marehemu Makwaya ambao walikuwa ni wafanyabiashara wa duka la pamoja walikwenda kwa mshtakiwa ili kupata dawa ya kuongeza utajiri wao ndipo mshtakiwa wa kwanza (Masasi) na mshtakiwa wa pili (aliyeachiwa baada ya kuonekana hana kesi), waliwaua na kisha kuwazika porini. Upande wa mashtaka uliita mahakamani mashahidi wanane ambao ni pamoja na mwenyekiti wa kijiji, maofisa wa polisi waliowatia mbaroni watuhumiwa na kupeleleza tukio hilo, mke wa marehemu Makwaya, daktari na mlinzi wa amani (Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Bagamoyo), ambaye mshtakiwa alitoa maelezo ya ungamo mbele yake. Mashahidi hao ambao maelezo yao yalifananafanana waliieleza mahakama kuwa mshtakiwa alikamatwa baada ya marehemu kupotea katika mazingira ya kutatanisha ambapo walianza kumfuatilia na kumkuta akiwa anaendesha baiskeli ya mmoja wa marehemu. Walisema mshtakiwa alipelekwa katika kituo cha polisi Chalinze ambako alihojiwa na kukiri kuwaua watu hao ndipo kesho yake alirudishwa kijijini pale akiwa na askari polisi pamoja na daktari na kwenda kuwaonyesha mahali alikokuwa ameizika miili ya marehemu wale, mbele ya viongozi wa kijiji. Walisema miili miwili ilikutwa imefukiwa katika shamba moja porini tofauti tofauti na kwamba mshtakiwa aliwapeleka sehemu nyingine ambako walikuta miili miwili iliyokuwa imefukiwa ndani ya kisima kilichokauka pamoja na mchi wa kutwangia. Walisema mwili mmoja wa mwanaume na mwingine wa mwanamke na kwamba miili yote hiyo ilikuwa na majereha kichwani. Mshtakiwa alipelekwa hospitalini kupimwa akili na baadaye akaandika maelezo yake ya onyo (Caution statement) mbele ya shahidi wa saba (ofisa wa polisi aliyepeleleza tukio hilo), kisha alipelekwa kwa mlinzi wa amani ambako aliandika maelezo ya ungamo (Confession Statement) ambako kote huko alikiri kuwaua watu hao. Mlinzi wa amani, Rehema Juma Salum ambaye ni shahidi wa nane aliileza mahakama kuwa mshtakiwa alitoa maelezo mbele yake kwa hiyari na kwamba alikiri kuwaua marehemu na kuwafukia, baada ya kuwapa dawa za kienyeji ili aweze kurithi mali zao kama vile mashamba, nyumba na biashara walizokuwa nazo kama vile duka. Hata hivyo, wakati akijitetea mahakamani mshtakiwa alikana mashtaka hayo na kwamba yeye si mganga wa kienyeji bali ni mkulima na mfugaji ambaye hufanya pia shughuli za biashara ya kuuza nyama. Alidai kuwa alikuja Chalinze Juni 2004 kutoka kwao Shinyanga ambako ameacha wake wanane na watoto 32, kwa ajili ya kununua ng'ombe ili awasafirishe kuja Dar es Salaam kwa njia ya reli na kwamba ndipo alipofuatwa na mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mwenyekiti wa kijiji na kumwambia kuwa anahitajika katika ofisi ya kijiji. Alidai akiwa huko ndipo alipokamatwa na polisi na kuchukuliwa begi lake lililokuwa na pesa Sh72milioni za biashara, huku akidai polisi walimpiga kwa muda wa siku tano ndipo siku ya sita walipompeleka hospitalini kutibiwa majeraha kabla ya kufikishwa mahakamani kwa mashataka hayo. Alikana pia kuandika maelezo ya onyo kwa polisi na ya ungamo kwa mlinzi wa amani, kuwafahamu wala kuishi kama wageni kwa marehemu hao wala kukiri kufanya mauaji hayo na kuwapeleka mashahidi hao eneo la matukio, huku akidai kuwa polisi walimbambikizia kesi hiyo ili wamdhulumu pesa zake hizo Sh72milioni alizokamatwa nazo. Hata hivyo, Jaji Sheikh alipuuza utetezi wake na kusema kuwa hauna msingi wala si wa kweli. Alisema kuwa wakati akitoa ushahidi wake alikuwa akimwangalia sana na mshtakiwa huyo alionekana kuwa ni mjanjamjanja na mkwepaji ambaye hakutaka kuisaidia mahakama.

No comments:

VJN Super Motors

Wauzaji Mahiri wa Spare za Pikipiki na Magari yote toka Europe na Japan, Tupo Mtaa wa Msikitini Musoma Mjini, Pia tunaweza kutoa hudumu kwa watu wa Dar es salaam, Wasiliana nasi kwa Sanduku la Barua 557 Musoma, Simu No. 0282620610 , Barua pepe : vincent_nye@yahoo.co.uk. Karibuni wote