
Wakati Polisi wameendelea kutoa kauli zenye utata juu ya kukamatwa kwa Mwandishi wa Habari za Uchunguzi wa TBC1, Jerry Muro, Baraza la Habari Tanzania (MCT), limetaka uchunguzi ufanyike haraka na kumfikisha mahakamani, ili ukweli wa tukio hilo ubainike kwani mazingira ya kukamatwa kwake yamejaa utata. Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, alisema kukamatwa kwa Muro kumegusa hisa za watu wengi hivyo ni muhimu ukweli ukajulikana mapema. Alisema MCT itamwekea mawakili wazuri wa kumtetea na alishauri vyombo vya dola vimchukulie Muro kama mtuhumiwa na si mhalifu hadi mahakama itakavyoamua vinginevyo. “Muro ni mwandishi bora wa mwaka na tutaendelea kumchukulia hivyo…Kazi alizoshinda zinahusu vita dhidi ya rushwa ndiyo maana kukamatwa kwake kwa tuhuma za rushwa kumetushtua sana, imetutia doa na imeacha maswali mengi kwa tasnia ya habari nchini na uaminifu wetu umetiwa shaka,” alisema. Alisema MCT inatambua kazi nzuri zinazofanywa na Muro na zitabaki kuwa nzuri na za kuigwa katika tasnia ya habari. Alisema kesi nzima imejaa utata na mambo hayako wazi hivyo kesi ichunguzwe haraka ili kubaini ukweli. “Hili suala lisipomalizwa mapema litatisha wandishi wa habari kufanya habari za uchunguzi..Vitisho na misukosuko katika habari za uchunguzi ni jambo la kawaida kokote duniani, lakini MCT haitakaa kimya kuona mtu anatumia cheo ama fedha zake kuwanyamazisha waandishi wa habari,” alisema Mukajanga. Aliongeza kuwa Muro alikuwa anakamilisha habari itakayogusa ufisadi wa baadhi ya mawaziri na vigogo, hivyo kukamatwa kwake lazima kutiliwe mashaka. Wakati huo huo, sakata la kukamatwa kwa Muro, akidaiwa kuomba rushwa kwa Mhasibu wa Halmashauri ya Bagamoyo, Michael Wage (50), limeingia katika sura mpya baada ya Muro kudaiwa kujitambulisha kwa mtu huyo kama mwanajeshi mwenye nyota tatu na kumtishia kwa silaha. Muro alikamatwa juzi asubuhi eneo la City Garden, muda mfupi baada ya Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kupata taarifa kutoka kwa mlalamikaji kuwa anatishiwa maisha na kuombwa rushwa na watu wanne. Kamanda wa Kanda hiyo, Suleiman Kova, alisema jana kuwa Muro akiwa na wenzake kabla ya tukio hilo walimtishia kwa silaha mlalamikaji na kumtaka atoe Sh. milioni 10 kwa lengo la kumsafisha dhidi ya kashfa inayomkabili. Kova alisema Muro alijitambulisha kama mwanajeshi kwenye nyota tatu wakati watuhumiwa wenzake watatu ambao wanaendelea kusakwa walijitambulisha kama maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Kaimu Kamanda wa taasisi hiyo. Kova alisema juzi majira ya asubuhi Wage alifika Polisi Kati na kutoa malalamiko dhidi ya watu hao kwamba wanamtishia kwa silaha na pingu kuwa yeye ni fisadi anayemiliki mali nyingi yakiwemo majumba ya kifahari na kutishia kumchukulia hatua za kisheria. Alisema Wage aliieleza polisi kuwa, watu hao walimtaka atoe Sh. milioni 10 ili waweze kumsaidia. “Wage alitueleza kuwa hayupo tayari kutoa fedha hiyo ndio maana amekuja kwetu kutoa taarifa juu ya tukio hilo, pia alitueleza kuwa, mwanajeshi huyo ana pingu na silaha anazotumia kumtishia na anadhani miwani yake (mlalamikaji) inaweza ikawa ndani ya gari la mtuhumiwa huyo baada ya kuisahau,” alisema. Alisema baada ya taarifa hiyo, mlalamikaji pamoja na makachero walifika City Garden ambapo mlalamikaji alimpigia simu Muro kuwa amefika eneo la tukio, lakini kutokana na mazingira hataweza kuingia ndani kama alivyokubaliana. “Tukiwa nje ya City Garden, mlalamikaji alimpigia simu mtuhumiwa (Muro), lakini kwa wakati huo hatukujua kama ni mtangazaji tulijua ni matapeli tu wa hapa mjini, ndipo alipotokea tulishangaa kumuona ni Jerry, tulimkamata kabla ya kitendo cha kupeana fedha hakijakamilika kutokana na ushahidi wetu kukamilika," alisema. Kova alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia gari namba T545 BEH Cresta 100 GX. Alisema wakati wakiwa eneo la tukio mlalamikaji (Wage) alitoa maelezo mbele ya makachero kuwa mtuhumiwa na wenzake watatu walikuwa wakimpa vitisho na kumtishia silaha. Kova alisema mlalamikaji aliwaeleza kuwa Januari 28, mwaka huu majira ya saa 12:00 jioni akiwa nyumbani kwake alifuatwa na watuhumiwa hao na kumtishia atoe rushwa. Alisema siku iliyofuata mtuhumiwa alikuwa akimpigia simu mara kwa mara kumkumbushia kuhusiana na makubaliano waliyofikia ndipo alipoamua kuja Dar es Salaam. “Kuhusu bunduki yenye namba CZ 97B namba A6466 iliyotengenezwa Jamhuri ya Czech inayomilikiwa na mtuhumiwa haina shida kwa sababu anaimiliki kihalali, lakini pingu aliyokutwa nayo ambayo alitueleza aliinunua pamoja na silaha hiyo lakini hapa nchini hakuna duka linalouza pingu," alisema. Alisema ushahidi walionao ni jinsi malalamikaji na mtuhumiwa walivyokuwa wakikutana. Alisema ushahidi huo ni kupitia kamera za CCTV ambazo zipo kwenye mahoteli ambayo watu hao walikuwa wakikutana. Alipoulizwa kwa nini walifanya haraka ya kumakata mtuhumiwa kabla ya kupokea rushwa hiyo, alisema walifanya hivyo kutokana na ushahidi wa kimazingira kukamilika. “Kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 292 kinasema mtu yeyote mwenye nia ya kuiba mali ya mtu akitoa madai kwa vitisho na kudhibitika ni kosa la jinai na hufungwa miaka mitano jela, pia kwa mujibu wa sheria ya Takukuru kifungu cha 15 kinasema kitendo cha kudai rushwa ni kosa, hivyo mazingira ya tukio yanatosha kuchukua hatua,” alisema. Kamanda Kova alisema ili kuondokana na dhana potofu kuwa labda tukio hilo limehusisha jeshi hilo wameamua upelelezi wao utakapokamilika jalada la kesi litapelekwa ofisi ya Wakili wa Serikali ambaye ndiye atatoa uamuzi wa kupelekwa mahakamani au la. Kova alisema tukio hilo hawakuwashirikisha Takukuru kwa sababu sio lazima kila tukio wafanye hivyo. “Lakini watuhumiwa wenyewe walijitambulisha kwa mlalamikaji kuwa ni maofisa kutoka Takukuru hivyo tuliamua kuifanya kazi hii wenyewe..lakini sio lazima kila suala la rushwa tuwashirikishe wao kwa sababu nasi tuna mamlaka ya kukamata watuhumiwa wa aina hiyo,” alisema. Baadaye jana jioni, Kova alitoa taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa wawili kati ya watatu waliokuwa wakitafutwa.
No comments:
Post a Comment