Uwepo wa Site hii Unategemea sana Ushirikiano wangu na wako, na ni njia mojawapo ya kuonyesha mshikamano na Jamii inayotuzunguka , PLS Usisite kunitumia Habari au kitu chochote chenye Uhakika ambacho hisia zako zitakupeleka kuwa kitaleta Mabadiliko na mafunzo katika jamii, Kumbuka kuwa msaada si Fedha wala Lulu bali chochote kinachoweza kuleta mabadiliko katika Maisha ya mtu mwingine. Kwa lolote usisite kuwasiliana nami kupitia chingasite@gmail.com au tumainijhn@yahoo.co.uk au simu No. 0712221744 na 0787221744. Karibuni Wote
Powered By Blogger

Friday, December 4, 2009

Kesi ya Babu Seya na Wanawe Utata mtupu, nini hatima yake? Je Haki ilitendeka au itatendeka?

MAWAKILI wanaomtetea mwanamuziki mahiri wa muziki wa dansi nchini, Nguza Viking maarufu ‘Babu Seya’ na wanawe watatu, wameiomba mahakama kuwaachia huru warufani kwa kuwa kesi hiyo ilikuwa ya kupangwa. Sambamba na hilo, mawakili hao; Mabere Marando na Hamidu Mbwezeleni, walieleza kuwa tangu waanze kazi ya uwakili miaka 30 iliyopita, hawajawahi kuona hukumu ya ovyo kama hiyo. Mawakili hao walieleza hayo jana mbele mbele ya jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Nataria Kimaro, walipokuwa wakiwasilisha sababu za kupinga rufaa ya Mahakama Kuu iliyolewa na Jaji Msaafu, Thimas Mihato na hukumu iliyotolewa na Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Addy Lyamuya ambao wote walitia hatiani kwa makosa ya kubaka. Majaji wengine wanaounda jopo hilo ni Salum Massati na Mbarouk Mbarouk. “Waheshimiwa majaji, sisi tunasema jaji na hakimu huyo walikosea kisheria, kwani sheria inaitaka mahakama kabla haijaanza kuchukua ushahidi wa mtoto ni lazima ijiridhishe mtoto huyo ana akili timamu na anaelewa maana ya kiapo na kisha irekodi hayo kwenye jalada la kesi, lakini Hakimu Lyamuya hakufanya hivyo. “Mashahidi 10 ambao ni watoto wadogo wenye umri kati ya miaka 6-8 ambapo upande wa mashitaka ulidai walibakwa na kulawitiwa na warufani, walipofika Mahakama ya Kisutu kutoa ushahidi wao hawakuhojiwa na wala mahakama haikujiridhisha kama wana akili timamu, kwa sababu hiyo tunasema kwamba ushahidi wa watoto hao ni batili na tunaliomba jopo lenu lisiukubali,” alidai Marando. Marando alidai kuwa wakati akitoa hukumu hiyo, Hakimu Lyamuya aliandika maoni yake binafsi ambayo yanapishana na mashahidi wa upande wa utetezi, kitu ambacho kinapingana na sheria za nchi. “Katika hukumu hiyo utaona wazi hakimu anabishana na shahidi baada ya kumbishia shahidi huyo kwamba si Mzaramo, wakati shahidi huyo aliiambia mahakama mama yake ni Mzaramo na baba yake ni Mkongo... haya ni mambo madogo, lakini yanaonyesha ni jinsi gani hakimu alivyopuuza ushahidi wa upande wa utetezi,” alieleza na kuongeza: “Waheshimiwa majaji sijawahi kuona hukumu kama hii kwa miaka 30 tangu nianze kazi ya uwakili, kwani sote tunachojua maoni ya hakimu katika hukumu yanaandikwa pembeni, lakini katika hukumu hii hakimu ameweka maoni yake,” alidai Marando na kusababisha watu kuangua vicheko. Akimuelezea mrufani Papi Kocha, alidai kuwa mrufani huyo alimweleza katika kipindi hicho alikuwa mikoani kwa ziara za kikazi, lakini hakimu Lyamuya katika hukumu yake akaweka mawazo yake kwa kusema hata kama alikuwa safari anaweza kutenda makosa hayo. “Lakini majaji katika rufaa ya Mahakama Kuu hakuna ushahidi uliotolewa unaoonyesha warufani walibaka... hayo yalikuwa ni mawazo ya hakimu kwamba lazima Babu Seya na watoto wake waende gerezani, narudia tena sijawahi kuona hakimu wa aina hii na hukumu ya aina hii ambayo hakimu aliamua kuweka maoni yake binafsi. “Ni wajibu wa mahakama kutafakari ushahidi wa utetezi hata kama hauna uzito, sasa huyu Lyamuya katika hukumu yake amewataja mashahidi wa utetezi waliokuja kutoa ushahidi bila kueleza mashahidi kwa mapana walieleza nini,” alidai. Aidha, alidai mmoja wa mashahidi wa upande wa upande wa mashitaka ambaye hakuapishwa, alidai shahidi huyo alifundishwa kusema uongo wa dhahiri kwani mtoto aliiambia mahakama walikuwa wakifundishwa Kiingereza na aliyekuwa mshitakiwa wa tano ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Mashujaa, Sigirinda Ligomboka ambaye aliachiliwa huru. “Ushahidi wake alidai Babu Seya alimbaka, lakini hakuna rekodi yoyote inayoonyesha shahidi huyo alimtaja. Shahidi huyo alitaja majina ya vijana waliomkamata ni Cheupe na Sembe na katika warufani hao hakuna mrufani mwenye majina hayo na upande wa mashitaka wala hawakuwaleta mahakamani watu hao, ili wawe mashahidi,” alidai Marando. Akiendelea kuuchambua ushahidi huo, alidai kuwa ushahidi huo unaonyesha kuwa mtoto huyo alikuwa akibakwa hata siku ambazo si za shule na kutoa mfano kuwa Oktoba 11, mwaka 2004 ilikuwa Jumamosi na tayari Babu Seya alikuwa ameishakamatwa, lakini shahidi huyo alieleza kuwa siku hiyo alikuwa amebakwa. Akichambua kwa ujumla ushahidi wa watoto hao, alidai kuwa hakuna shahidi wa upande wa mashitaka aliyeiambia mahakama kuwa makosa hayo yalitendekea Aprili, Mei, Juni, Julai, Agosti, Septemba na Oktoba isipokuwa hati ya mashitaka inasomeka kwamba makosa yote yalitendeka kati ya Septemba na Oktoba, lakini juaji na hakimu huyo wakaridhia. Aidha, alidai mmoja wa watoto hao alidai kubakwa hadi kutoka damu, lakini taarifa ya daktari iyowasilishwa mahakamani hapo ilionyesha kuwa mtoto huyo ni bikira na wala haonyeshi aliwahi kubikiriwa wala kuingiliwa kinyume na maumbile. Pamoja na hayo, alihoji kilichofanya upande wa mashitaka kuficha ripoti ya daktari aliyewafanyia uchunguzi watoto hao wanaodaiwa walibakwa na kushindwa kuleta mashahidi ambao ni wanamuziki wa bendi ya Achigo, mama wa Babu Seya na mke wa Babu Seya kwa sababu waliona mashahidi hao wangewaumbua. “Kesi hii ni ngumu kwetu sote na kama mahakama na sisi tunaona warufani walifanya haya makosa tuwalaani ila mimi Marando nasema nimejiridhisha hawajafanya hayo makosa. “Hivi tujiulize, kibaiolojia kweli inawezekana mtoto wa miaka sita abakwe na wanaume hawa (warufani) nyuma na mbele halafu mtoto huyo aweze kutembea? Haiingii akilini hata kidogo, nasema kesi hii ni ya kutunga, kwani hata mwanamke mwenye umri wa utu uzima akifanyiwa unyama huo hawezi kutembea,” alidai Marando. Akijibu hoja za mrufani, wakili Mkuu wa Serikali Justus Mulokozi, alidai kitendo cha shahidi kushindwa kumtambua mshitakiwa mahakamani si sababu inayosababisha ushahidi wa shahidi huyo kuonekana hauna thamani, jibu lililosababisha umati wa watu kuangua vicheko. Mulokozi alidai pia mahakama ikiamini upande mmoja, hailazimiki kuangalia upande mwingine, hoja ambayo ilipingwa na Marando ambaye alidai kuwa hoja hiyo haikupaswa kutolewa na wakili mwandamizi kama Mulokozi kwani hoja hiyo inatofautiana na sheria za nchi na kauli ya wakili huyo wa serikali imedhihirisha ni kweli Lyamuya aliegemea ushahidi wa upande wa mashitaka. Jaji Kimaro alisema jopo hilo tayari imeishamaliza kusikiliza rufaa hiyo na akasema jopo lake litatoa taarifa ya hukumu.

No comments:

VJN Super Motors

Wauzaji Mahiri wa Spare za Pikipiki na Magari yote toka Europe na Japan, Tupo Mtaa wa Msikitini Musoma Mjini, Pia tunaweza kutoa hudumu kwa watu wa Dar es salaam, Wasiliana nasi kwa Sanduku la Barua 557 Musoma, Simu No. 0282620610 , Barua pepe : vincent_nye@yahoo.co.uk. Karibuni wote