Uwepo wa Site hii Unategemea sana Ushirikiano wangu na wako, na ni njia mojawapo ya kuonyesha mshikamano na Jamii inayotuzunguka , PLS Usisite kunitumia Habari au kitu chochote chenye Uhakika ambacho hisia zako zitakupeleka kuwa kitaleta Mabadiliko na mafunzo katika jamii, Kumbuka kuwa msaada si Fedha wala Lulu bali chochote kinachoweza kuleta mabadiliko katika Maisha ya mtu mwingine. Kwa lolote usisite kuwasiliana nami kupitia chingasite@gmail.com au tumainijhn@yahoo.co.uk au simu No. 0712221744 na 0787221744. Karibuni Wote
Powered By Blogger

Friday, December 11, 2009

Mtuhumiwa wa Mauaji ya mkewe mtarajiwa na mama mkwe atoroka akiwa chini ya ulinzi wa polisi

Mtuhumiwa wa mauaji ya watu wawili na yeye kujaribu kujichinja koromeo ametoroka akiwa katika hospitali teule ya DDH, Serengeti, huku akiwa chini ya ulinzi. Mtuhumiwa huyo ametoroka wakati akiwa amepewa rufaa kwenda Bugando kwa matibabu. Tukio hilo linadaiwa kuwa ni la pili kwa askari magereza kutorokwa na mtuhumiwa wa mauaji hapo hospitali, hali ambayo inaibua maswali mengi huku uongozi wa jeshi hilo ukiwa kimya. Habari za uchunguzi zimebaini kuwa Muyuga Maduhu (25), mkazi wa kijiji cha Rigicha aliyekuwa anakabiliwa na mashitaka ya kuwaua watu wawili; mama mkwe wake mtarajiwa, Mageni Masaka (60) na mchumba wake, Suzana Chande Makanika (30) kwa kuwakatakata kwa panga kutokana na wivu wa mapenzi, alitoroka hospitalini hapo akisubiri kupelekwa Bugando kwa matibabu zaidi. Mshitakiwa huyo ambaye tayari alikuwa ameshasomewa mashitaka mawili ya mauaji akiwa kitandani alikabidhiwa kwa askari magereza baada ya kusomewa mashitaka na alikuwa chini ya uangalizi wao kwa muda wote. Habari kutoka vyanzo vya habari hospitalini hapo zimedai kwamba Maduhu anayedaiwa kutenda unyama huo Novemba 4, mwaka huu, saa 7:00 usiku, alisomewa mashitaka Novemba 6 kisha akakabidhiwa kwa askari magereza ambao walikuwa wakipeana zamu kumlinda na inaelezwa kwamba muda wote alikuwa amefungwa pingu kitandani. Inaelezwa kwamba wakati muda wote Maduhu alikuwa kwenye pingu hata anapokwenda chooni, siku ya tukio askari aliyekuwa akimlinda alimfungua pingu zote na kumwacha aende pekee yake chooni. Inasemekana kwamba askari huyo, jina tunalo, alikuja kushtuka baadaye kwamba hamuoni mshitakiwa na kujaribu kuwauliza wauguzi ambao pia walibaki kushangaa kuhusu aliko Maduhu ambaye alitakiwa kupelekwa Bugando kwa matibabu ya koo na ambaye hakuna ndugu hata mmoja aliyekuwa anafika kumwona. Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Amos Kittoh, alipoulizwa anachojua kuhusu kutoroka kwa mfungwa huyo alijibu: "Nilikuwa likizo, sikuwa najua lakini nafahamu kuwa alitakiwa kwenda Bugando, maana hali yake haikuwa nzuri. Kama ametoroka na kama hatopata matibabu ni maajabu kunusurika kifo... Lakini nitafuatilia,” alisema. Uongozi wa magereza hapa Serengeti haukuwa tayari kuzungumzia suala hilo na juhudi za kumsaka mkuu wa magereza mkoa wa Mara zinaendelea. Kabla ya kujaribu kujiua Novemba 4 baada ya kumuua mkewe na mkwewe, Maduhu alitia kiberiti nyumba yao, kisha akajitundika kwa kamba lakini kamba ilipokatika, ndipo akachukua kisu na kujichinja koromeo. Sababu ya Maduhu kufanya ukatili huo inadaiwa kwamba ni baada ya mkewe kumkataa na kurudi kwao na alipofuatilia ili mama mkwe wake arejeshe sh. 50,000 alizokuwa ametoa kama kishika uchumba, alikataliwa na ndipo akaamua kufanya unyama huo.

No comments:

VJN Super Motors

Wauzaji Mahiri wa Spare za Pikipiki na Magari yote toka Europe na Japan, Tupo Mtaa wa Msikitini Musoma Mjini, Pia tunaweza kutoa hudumu kwa watu wa Dar es salaam, Wasiliana nasi kwa Sanduku la Barua 557 Musoma, Simu No. 0282620610 , Barua pepe : vincent_nye@yahoo.co.uk. Karibuni wote