Uwepo wa Site hii Unategemea sana Ushirikiano wangu na wako, na ni njia mojawapo ya kuonyesha mshikamano na Jamii inayotuzunguka , PLS Usisite kunitumia Habari au kitu chochote chenye Uhakika ambacho hisia zako zitakupeleka kuwa kitaleta Mabadiliko na mafunzo katika jamii, Kumbuka kuwa msaada si Fedha wala Lulu bali chochote kinachoweza kuleta mabadiliko katika Maisha ya mtu mwingine. Kwa lolote usisite kuwasiliana nami kupitia chingasite@gmail.com au tumainijhn@yahoo.co.uk au simu No. 0712221744 na 0787221744. Karibuni Wote
Powered By Blogger

Monday, December 7, 2009

Mambo usiyoyajua kuhusu Ernest Semayoga - Mfungwa aliyepata Digrii ya Sheria akiwa kifungoni

Semayoga (37) ambaye ni kijana mtanashati aliyezaliwa mwaka 1972, alitunukiwa shahada hiyo na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk. John Malecela katika hafla ya pekee iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Tolly Mbwete, Waziri wa Mambo ya Ndani Lawrence Masha, Mkuu wa Magereza, Kamishna Augustino Nanyaro na wafanyakazi mbalimbali wa OUT na Magereza. Sherehe hiyo iliyopambwa na bendi ya Polisi pia ilihudhuriwa na ndugu wa Semayoga, waandishi wa habari pamoja na wanajeshi waliokuwa wakitumbuiza katika hafla hiyo kwa bendi yao. Semayoga, ni mmoja wa wahitimu wa mwaka huu wa Chuo Kikuu Huria (OUT) katika sehemu ya pili ya Mahafali ya 21 ya chuo hicho yaliyofanyika katika viwanja vya Kikosi Maalumu cha Kuzuia Ghasia Magerezani, Ukonga, Ilala, jijini Dar es Salaam. Mahafali hayo yalifanyika katika nyakati mbili tofauti ambapo mfungwa huyo alifanyiwa ya kwake Desemba mosi tofauti na wahitimu wenzake waliofanyiwa ya kwao Novemba mwaka huu kutokana na masharti ya Sheria za Magereza. Kijana huyo mwenye mke na mtoto mmoja anayeitwa Astrida Michael anayesoma kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya St. Mary iliyoko Mbezi jijini Dar es Salaam alipopata wasaa wa kuzungumza, baada ya kupata shahada yake kwa kujiamini aliiomba serikali iwasamehe wafungwa waliojirekebisha. Mfungwa huyo anayetarajia kumaliza kifungo chake Agosti mwakani, anasema mfungwa aliyeonesha kujifunza na kujirekebisha anaposamehewa, husaidia kuwashawishi wafungwa wengine kubadili tabia na kujiandaa kwa ajili ya maisha yao baada ya kutoka gerezani. Semayoga ambaye ana ndoto za kujiunga na Shahada ya Uzamili ya Sheria (LLM), anaelezea historia yake kuwa alizaliwa mkoani Kigoma na kusoma Shule ya Msingi ya Kigoma mnamo mwaka 1981 hadi 1987 na alipomaliza darasa la saba, alichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari ya Kilosa alikosoma kidato cha kwanza na pili. Alipofika kidato cha tatu alihamia Shule ya Sekondari Kigoma alikomaliza kidato cha nne mwaka 1991 na kufanikiwa kujiunga na kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Azania alikokuwa akichukua masomo ya Fizikia, Kemia na Biolojia (PCB). Alimaliza kidato cha sita mwaka 1994 lakini hakufanikiwa kuendelea na elimu ya juu kwa kuwa alifiwa na mama yake mzazi msiba ambao anasema ulisababisha achanganyikiwe na kushindwa kuendelea na shule. “Baada ya muda nilianza kufanya biashara mbalimbali na baadaye nilishawishika kufanya biashara haramu ya kuuza dawa ya kulevya toka nchini Mauritius kwenda Afrika Kusini na Tanzania,” anasema. Mwaka 1999 akiwa njiani kutoka nchini Afrika Kusini kuja Tanzania kupitia Mauritania akiwa na dawa za kulevya, alikamatwa na kufungwa nchini humo hadi mwaka 2006 aliporejeshwa nchini Tanzania kuendelea na kifungo chake. Anasema alifikia katika Gereza la Ukonga na mwaka 2007 ambapo aliamua kujiunga rasmi na OUT kuchukua masomo ya sheria ili kusaidia wafungwa kwa kuwa hawafahamu haki na taratibu zao na kuongeza kuwa amekuwa akiwasaidia kuandaa rufaa zao. Anasema kaka yake mkubwa Dk. Francis Semayoga, ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ndiye aliyemhamasisha kuanza masomo katika chuo hicho na kwa kushirikiana na OUT walimpatia vitabu na vifaa mbalimbali vya kusoma. Akizungumzia changamoto anazopata anasema kubwa aliyokabiliana nayo ni pamoja na kutokuwa na muda maalumu wa kusoma kwa kuwa ni lazima kufuata taratibu za gerezani ambapo anapaswa kulala saa tisa mchana, ingawa kwa sasa magerezani hali imebadilika siyo kama ilivyokuwa hapo zamani, lakini dhana ya kurekebisha watu tabia inatakiwa kuboreshwa ili anapotoka gerezani, awe mtu mpya. Anasema serikali inapaswa kuboresha mazingira ya kusoma kwa ajili ya wafungwa kwa sababu wapo wengi wanotamani kusoma lakini hawajafikia kiwango cha elimu kinachohitajika wakubalike kujiunga na elimu ya juu. Dada mkubwa wa Semayoga, Theobaldina Kasakanta anasema Semayoga ambaye ni mdogo wao wa sita na ni kati ya kaka zao wanne na dada watatu ambapo mmoja alifariki mwaka jana. Anasema wanamshukuru Mungu kwa hatua aliyoifikia mdogo wao kwa kuwa wamepata faraja kwani baada ya kufungwa waliona wamempoteza lakini kwa sasa baada ya kupata shahada, wanaamini akimaliza kifungo atakuwa mtu mpya katika familia. Anasema tangu utoto wake Semayoga hakuwa na makuu na kwamba siku zote alikuwa na upendo. Anasema kasoro iliyojitokeza ya kujiingiza katika biashara ya dawa za kulevya ilisababishwa na kudanganyika tu akiwa katika jitihada za kutafuta maisha. Hata hivyo dada huyo anasema yeye na ndugu wengine wamefanikiwa kuhudhuria mahafali hayo lakini mkewe Semayoga yuko masomoni nchini Marekani na mtoto wake yuko katika ziara ya kimasomo mkoani Morogoro na hivyo hawakuhudhuria. Rafiki wa Semayoga aliyetoka katika mji wa Kahama mkoani Shinyanga kushuhudia mahafali hayo ambaye pia anaitwa Ernest waliyesoma naye Shule ya Sekondari ya Kilosa, anasema rafiki yake huyo alikuwa na akili sana katika masomo huku akipenda kila mwanafunzi aelewe. Anasema mara kwa mara nyakati za jioni wanafunzi wenzake walimfuata kuomba awafundishe kile walichokuwa hawajaelewa. Anasema anahisi kitendo cha rafikiye kujiingiza kuuza dawa za kulevya kilikuwa cha bahati mbaya akiwa katika kutafuta maisha.

2 comments:

Anonymous said...

What is he gonna do now!! a felony lawyer.

Good he got a degree,but you guys blew this out of proportions.

He should feel remorse by pushing illegal drugs that destroys many families.

You people should ask him how is he gonna help anti drugs force and public in general in fighting against drug calamity?

Anonymous said...

What is he gonna do now!! a felony lawyer.

Good he got a degree,but you guys blew this out of proportions.

He should feel remorse by pushing illegal drugs that destroys many families.

You people should ask him how is he gonna help anti drugs force and public in general in fighting against drug calamity?

VJN Super Motors

Wauzaji Mahiri wa Spare za Pikipiki na Magari yote toka Europe na Japan, Tupo Mtaa wa Msikitini Musoma Mjini, Pia tunaweza kutoa hudumu kwa watu wa Dar es salaam, Wasiliana nasi kwa Sanduku la Barua 557 Musoma, Simu No. 0282620610 , Barua pepe : vincent_nye@yahoo.co.uk. Karibuni wote