
WAFANYAKAZI wa Kampuni ya Reli nchini (TRL), kwa mara ya kwanza, jana walivamia na kuteka ofisi za menejimenti ya kampuni hiyo kwa saa kadhaa ili kushinikiza kulipwa mishahara yao ya Novemba, mwaka huu. Hatua hiyo ilifikiwa na wafanyakazi hao baada ya menejimenti ya TRL kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kuwalipa mishahara yao kwa madai kuwa amenunua vifaa na pato la kampuni limeshuka. Akizungumza katika kikao cha dharura ilichofanyika katika karakana ya TRL kati ya wafanyakazi na viongozi wa Chama cha wafanyakazi wa Reli (TRAWU), Katibu Mkuu wa chama hicho, Sylvester Rwegasira alieleza kusikitishwa na majibu yanayotolewa na menejimenti ambayo yanaonesha jeuri. Alisema baada ya kurudi tena kwa menejimenti hiyo ili kujua lini watalipwa mishahara yao, majibu waliyopata hayakuwa ya kuridhisha kwani ilisisitiza haina fedha za kuwalipa wafanyakazi kwa sasa. “Kweli kama jana mlivyotutuma tulihakikisha majibu yote tunayarudisha kwenu na kwa hiyo menejimenti imesema haina fedha labda baada ya siku tano, wataangalia kama kuna uwezekano,” alisema Rwegasira. Baada ya tangazo hilo, wafanyakazi hao walishindwa kujizuia na kuamua kwenda kuonana na uongozi wa TRL. Ilipofika majira ya saa kumi jioni, wafanyakazi hao waliondoka kwa maandamano kutoka katika karakana hiyo kuelekea ofisi za menejimenti ambazo zipo karibu na ofisi za Mamlaka ya Mapato (TRA). Baada ya kufika katika eneo la ofisi hizo za menejimenti, walinzi walijaribu kuwazuia ili wasiingie ndani, lakini walipoona kundi kubwa la watu nje, waliamua kutulia. Aidha, wafanyakazi hao waliingia katika eneo la ofisi hizo huku wakisema kwa sauti kubwa kwamba wanahitaji mishahara yao. Viongozi waliokuwa ndani ya ofisi hizo baada ya kuona hali hiyo, kila mmoja alitoka kwa stahili yake na kukimbilia ghorofa ya juu ya ofisi hizo. Wakiwa na hasira, wafanyakazi hao waliamua kutoa upepo wa baadhi ya magari ya viongozi wa menejimenti hiyo yaliyokuwepo katika eneo hilo. Magari yaliyotolewa upepo ni yenye namba za usajili T 760 AWG, T 898 AZX, T 923 AVA, T 180 AUN, T 405 AVL na T 199 AZY. Hata hivyo, ilipofika majira ya saa kumi, menejimenti na viongozi wa TRAWU waliingia katika kikao cha dharura, huku menejimeti hiyo ambayo iliongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Hundi lal Chandhary ikiwataka waandishi wa habari kutoka nje na kuwaachia nafasi ya kuendelea na mazungumzo. Hata waandishi walipotoka, bado kikao hicho hakikuweza kufikia mwisho kwani baada ya dakika zisizopungua 20, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Reli, Ruth Makelemo, akiongozana na viongozi wa TRAWU, walitoka na kuelekea katika ofisi za Ukaguzi na Usimamizi wa Shughuli za Reli (RAHCO). Hata hivyo, muda wa kazi ulikuwa umekwisha na asilimia kubwa ya viongozi wa juu wa RAHCO walikwishaondoka hivyo waliweza kuonana na viongozi wa chini waliokuwepo hatua ambayo haikuweza kusaidia lolote. Haikujulikana mara moja walienda katika ofisi hizo kufanya nini. Wakati hayo yakiendelea, menejimenti haikuonekana kujishughulisha na lolote wala kuwajali wafanyakazi waliobaki katika eneo la ofisi zao, huku viongozi wa chama chao wakiendelea kuhaha kutafuta haki. Baadaye walirudi tena kuendelea na kikao hicho lakini hakuna lililofikiwa kwani hazikuzidi dakika 20, Rwegasira akiambatana na wenzake walitoka ili kuzungumza na wafanyakazi, waliokuwa muda wote wakisubiri hatma yao. Akitumia lugha ya busara, aliwaomba wafanyakazi hao kuendelea kuwaamini viongozi ambao hawataondoka mpaka wahakikishe wanapata mishahara yao. “Kweli tumeonyesha ushirikiano na naombeni kwa umoja huo huo muendelee kutuamini na hatutachoka, sisi tutakesha leo (jana) mpaka kieleweke,” alisisitiza. Alisema kama ni kazi, sasa ndiyo imeanza na juhudi bado zinahitajika, hivyo aliwataka wafanyakazi kutokata tamaa kwani wanafanya mawasiliano na serikali kujua hatma yao. Hatua hiyo iliwaridhisha wafanyakazi hao ambapo leo asubuhi wamepanga kukutana tena katika eneo hilo ili kupata majibu ya hatma ya mishahara yao. Wakati menejimenti ikigoma kutoa mishahara kwa wafanyakazi hao, tayari serikali imeshachangia sh milioni 522 kwa ajili ya kuwalipa. Hivi sasa wafanyakazi hao wanaitaka serikali kuvunja mkataba wa kampuni hiyo wa miaka 25 kwani hauna tija na imeonyesha kila dalili ya kushindwa.
No comments:
Post a Comment