

Waziri mkuu wa Italia Silvio Berlusconi amekumbana na kitu asichokitegemea maishani mwake baada ya kushushiwa kipigo mtaani kilichobabisha apoteze meno mawili. Mwanaume mmoja anashikiliwa na polisi nchini Italia baada ya kumshambulia waziri mkuu wa nchi hiyo Silvio Berlusconi na kumjeruhi usoni na kupelekea meno yake mawili yang'oke.Katika tukio hilo lililotokea jana jumapili asubuhi, wasaidizi wa Berlusconi mwenye umri wa miaka 73 waliwahi kumuokoa bosi wao asijeruhiwe zaidi na walimwahisha kwenye gari lake huku akivuja damu usoni. Aliwahishwa hospitali ambako anatarajiwa kukaa kwa masaa 24."Niko poa , niko poa", alinukuliwa akisema Berlusconi na shirika la habari la ANSA wakati alipokuwa akitoka kwenye chumba cha dharura cha hospitali.Mwanaume aliyemshambulia alikamatwa na kupelekwa makao makuu ya polisi ya mjini Milan.Taarifa zilizotolewa baadae zilisema kuwa mwanaume huyo alikuwa na historia ya matatizo ya akili kwa miaka 10.Waziri wa ulinzi Ignazio La Russa, ambaye alikuwa karibu na Berlusconi wakati wa shambulio hilo alisema kuwa waziri mkuu alikuwa akivuja damu puani na mdomoni. ANSA lilimkariri mmoja wa madaktari akisema kuwa meno mawili ya Berlusconi yaling'oka katika shambulio hilo.Berlusconi alikumbwa na zahama hilo wakati wa maandamano ya kisiasa yaliyofanyika jijini Milan.Berlusconi alikumbwa na tukio kama hilo miaka michache iliyopita wakati kijana mmoja mdogo alipomshambulia kwa kumpiga na chuma la stendi ya kamera na kusababisha apate jeraha kichwani kwake.Berlusconi amekuwa kwenye presha kubwa kuhusiana na maisha yake binafsi na maisha yake ya kisiasa akishutumiwa kufanya ubadhirifu serikalini.Pamoja na shinikizo hilo, Berlusconi, ambaye alishinda uchaguzi mwezi mei mwaka jana amesisitiza kuwa hataitisha uchaguzi mapema kabla ya muda wake.
No comments:
Post a Comment